Waiguru adai msimamo wake kuunga BBI ndiyo sababu ya 'masaibu'
Na CHARLES WASONGA
GAVANA wa Kirinyaga Anne Waiguru sasa anadai kuwa anaandamwa kwa sababu ya kuwa mkeretetwa sugu wa Mpango wa Maridhiano (BBI) katika eneo la Mlima Kenya.
Katika taarifa yake ya mwisho mbele ya kamati maalum ya seneti iliyodadisi iwapo tuhuma kwenye hoja ya kumwondoa afisi zina mashiko au la, Waiguru pia alisema hoja dhidi iliwasilishwa dhidi yake kwa sababu anaunga mkono muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.
“Msimamo wangu katika siasa za kitaifa umenifanya kuwa adui wa watu wenye ushawishi ndani na nje ya kaunti yangu. Ukweli ni kwamba ninashambuliwa kwa kuunga mkono BBI na handisheki,” Waiguru akasema Jumatano jioni.
Gavana huyo aliiomba kamati hiyo ya wanachama 11 inayoongozwa na Seneta wa Kakamega Cleophas Malala, kutupilia mbali hoja hiyo akiitaja kama iliyosheheni chuki na madai yasiyo na msingi wowote.
Hoja hiyo ilipitishwa Juni 9, 2020, na madiwani 23 kati ya 33 wa bunge la kaunti ya Kirinyaga, katika kikao kilichojaa fujo.
Bi Waiguru akaongeza: “Hii ni njama ya watu kutoka nje wakishirikiana na viongozi fulani wa Kirinyaga ambao nia yao ni kuvuruga shughuli za serikali ya kaunti. Naomba jambo kama hili lisiruhusiwe kushuhudiwa tena.”
Gavana huyo alisema madiwani walifeli kuthibitisha mashtaka dhidi yake, akiongeza kuwa yamesheheni uvumi na chuki na hivyo hayatimizi vigezo kwenye kikatiba vya kumwondoa gavana afisini.
“Baada ya kusikiza mawasilisho ya bunge la kaunti, ni dhahiri kuwa wametegemea mashahidi ambao walijaa hamaki na hivyo kutoa taarifa za kukanganya na ambao haukuandamanishwa na ithibati yoyote,” Bi Waiguru akasema.
Alisisitiza kuwa hakuwa na hatia, kwani mawakili wake, Paul Nyamodi na Kamotho Waiganjo, waliweza kuthibitisha kuwa hoja hiyo ya kumwondoa mamlakani haikuwa na mashiko yoyote.
“Mawakili wangu wamekosoa madai ya uongo yaliyotegemewa kupitisha hoja ya kuniondoa mamlakani. Na tumethibitisha kuwa hayaafiki utaratibu wa kumwondoa gavana afisini kama ulivyoelezwa kwenye Katiba. Masuala yaliyoibuliwa yangefafanuliwa kupitia taratibu za kawaida,” Bi Waiguru akasema.
Wanachama wa kamati hiyo walikamilisha vikao vya kuwahoji mashahidi kutoka pande mbili husika na itaandaa ripoti itakayowasilisha mbele ya kikao cha seneti kesho Ijumaa.