Watu 64 wakiwa kwa magari ya wamiliki binafsi wanaswa wakijaribu kukiuka zuio
Na LAWRENCE ONGARO
ABIRIA wapatao 64 walinaswa katika kizuizi cha Chania katika mpaka baina ya mji wa Thika na Kaunti ya Murang’a wakitoka jijini Nairobi.
Wakati huo pia magari madogo 10 ya wamiliki binafsi yalizuiliwa kwa sababu yalikuwa yamebeba abiria.
Kamanda mkuu wa polisi katika Kaunti ya Murang’a, Bw Josephat Kinywa, alisema maafisa wa polisi wataendelea kuweka doria ili kuwazuia wasafiri kuvuka kizuizi hicho kwa lengo la kupita.
Bw Kinywa alisema wasafiri hao walikosa stakabadhi maalum za kuwaruhusu kupitia katika kizuizi hicho.
“Baada ya kuhojiwa ilibainika ya kwamba wasafiri hao walitoka Nairobi kuelekea Nyeri, Meru, Isiolo, na maeneo mengine tofauti,” alisema afisa huyo.
Alisema hata kuna wasafiri wengine ambao walijaribu kupenya kizuizi hicho kwa kutumia bodaboda.
Alisema hata wengine walinaswa wakijaribu kuhonga maafisa wa polisi ili wapite kizuizi hicho cha Chania, kilichoko mpakani mwa Thika na Kaunti ya Murang’a.
Alisema wasafiri hao walionaswa watafikishwa mahakamani mara moja ili kujibu mashtaka ya kukiuka sheria za zuio la kusafiri baina ya baadhi ya maeneo wakati huu wa janga la Covid-19.
Afisa huyo alisema maafisa wa usalama hawatawaruhusu wasafiri kupitia vizuizi vinavyowekwa katika sehemu tofauti.
“Tumegundua ya kwamba wahudumu wa bodaboda wanaendesha biashara ya kuwavukisha wasafiri katika barabara za vichochoroni. Yeyote atakayenaswa atajilaumu mwenyewe, kwani hatutawaruhusu kupita,” alisema afisa huyo.
Katika Kaunti ya Kiambu kuna vizuizi vitatu muhimu ambavyo vinalindwa kwa muda wa saa 24 na maafisa.
Vizuizi hivyo ni kile cha Maryhill hadi Gatundu, kingine ni cha Kilimambogo kuelekea Kaunti ya Machakos na Murang’a halafu hicho cha Chania eneo la Bluepost, mjini Thika, kuelekea Nyeri, Meru, Isiolo na kwingineko.
Serikali pia imechukua jukumu la kutumia mitambo ya droni ili kuwasaka watu wanaopitia njia za mkato ili kuhepa walinda usalama.
Marufuku ya kutoingia na kutoka jijini Nairobi, na Mombasa iliwekwa na serikali karibu miezi miwili sasa huku Wakenya wengi wakitarajia mambo kubadilika mwezi ujao wa Julai, 2020.