Habari Mseto

Ningali seneta wa Kakamega – Malala

June 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

SAA chache baada ya chama cha Amani National Congress (ANC) kumfurusha, Cleophas Malala anashikilia kuwa angali Seneta wa Kaunti ya Kakamega.

Akiongea katika Seneti baada ya kuwasilisha ripoti kuhusu uchunguzi wa madai yaliyomo kwenye hoja ya kumwondoa mamlakani Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru; ripoti ambayo ilimwondolea lawama, Bw Malala aliwataka wenzake wawe watulivu na kuupuzilia mbali tangazo la ANC kwamba kimemfukuza.

“Na ninataka kusisitiza hapa kwamba mimi bado ndiye Seneta wa Kakamega licha ya habari zinazoenea huko nje kwamba watu fulani wamenifukuza kutoka ANC,” akasema.

Uamuzi huo uliafikiwa katika mkutano wa Baraza la Uongozi (NGC) la ANC ulioongozwa na kiongozi wa chama hicho Musalia Mudavadi.

Bw Malala anatuhumiwa kukiuka Katiba ya chama hicho na sheria ya vyama vya kisiasa kwa kumpigia debe mgombeaji wa ODM Imran Okoth ilhali ANC ilidhamini Bw Eliud Owalo katika uchaguzi huo mdogo eneobunge la Kibra mwishoni mwa mwaka 2019.

Aidha, anakabiliwa na tuhuma za kumkosea heshima kiongozi wa ANC Bw Mudavadi kwa kudai kuwa anamtambua Raila Odinga kama kiongozi wake katika ulingo wa siasa.

ANC ilisema kuwa ilifuata sheria na taratibu zifaazo kwa kumwamuru Seneta Malala afike mbele ya Kamati yake ya Nidhamu ili ajitetee dhidi ya madai hayo lakini akadinda.

Baadaye kamati hiyo ilikutana na kuamua kumfurusha Seneta Malala kutoka chama cha ANC.

“Matamshi yake na mienendo wakati wa mkutano wa kampeni ulioitishwa na ODM katika eneobunge la Kibra mnamo Oktoba 27, 2019, yalihujumu heshima na hadhi ya chama cha ANC, Kiongozi wake, wanachama na wafanyakazi wake,” kamati hiyo ilisema na hapo ikapendekeza Malala atimuliwe.

Mbunge Maalum wa ANC Godfrey Osotsi alidai hatua hiyo ni batili kwa sababu, kulingana naye, mkutano wa NGC uliopitisha kufurushwa kwa Seneta Malala “haukuitishwa kisheria.”

“Hatua hii ni mzaha. Kundi la watu ambao hawako afisini kisheria haliwezi kutoa maamuzi kama hayo. Uamuzi kama huu unaweza tu kutolewa baada ya ANC kuanza uchaguzi kwani muda wa kuhudumu wa viongozi wa sasa, akiwemo Bw Mudavadi, ulikamilika mnamo Juni 15, 2020,” Bw Osotsi akaambia Taifa Leo kwa njia ya simu.