• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
Magoha ataka taasisi za kozi za ufundi zifunguliwe Septemba

Magoha ataka taasisi za kozi za ufundi zifunguliwe Septemba

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Elimu Prof George Magoha amesema Vyuo vya Kozi za Ufundi Nchini (TVET) vitafunguliwa Septemba ili wanafunzi wafanye mitihani.

Akiongeza Ijumaa alipokutana na wakuu wa vyuo hivyo mjini Kisumu, waziri Magoha alisema mipango imewekwa kuhakikisha kuwa wanafunzi wanafanya mitihani kwa awamu.

Prof Magoha alisema hiyo itafanyika baada ya vyuo hivyo kufanyiwa ukaguzi kubaini kuwa vimejiandaa kwa utekelezaji wa kanuni za kuzuia kuenea kwa ugonjwa hatari wa Covid-19.

“Tafuteni wataalamu kutoka Wizara ya Afya ambao watawaelekeza kuhusiana na yale ambayo mnapaswa kufanya ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona. Bila haka nina imani kwamba mtafikia masharti hayo kwa sababu vyuo vyenu vina nafasi ya kufanikisha utekelezaji wa kanuni ya kutokaribiana sana,” akawaambia wakuu hao waliohudhuria mkutano huo katika Chuo Anuwai cha Kitaifa cha Kisumu.

Akaeleza: “Ikiwa Katibu wa Wizara ya Afya na maafisa wake watakagua vyuo vyenu na kuthibitisha kuwa vimezingatia kanuni za Covid-19, wanafunzi wanaweza kuruhusiwa kurejea ili wafanye mitihani.”

Waziri alishauri wakuu hao wa vyuo vya TVET kuweka mipango ya kuhakikisha kuwa wananunua barakoa za kutosha ambazo zitatumiwa na wanafunzi pamoja na wakufunzi.

Hata hivyo, Prof Magoha aliungama kuwa utekelezaji wa kanuni ya kutokaribiana na kutotangamana kiholela katika shule za msingi na za upili itakuwa kazi ngumu zaidi endapo maambukizi hayatakuwa yamepungua ifikapo Septemba.

You can share this post!

Sanitaiza ya BBI yang’arisha Waiguru

Manchester City waruhusiwa kuandaa gozi dhidi ya Liverpool...

adminleo