Michezo

Pedro Rodriguez kuagana na Chelsea na kujiunga na AS Roma

June 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI Pedro Rodriguez wa Chelsea atajiunga rasmi na AS Roma ya Italia baada ya mkataba wake uwanjani Stamford Bridge kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu.

Nyota huyo mzawa wa Uhispania ametia saini mkataba wa miaka miwili na miamba hao wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) katika maelewano yatakayomshuhudia akitia mfukoni kima cha Sh7 milioni kwa wiki.

Roma watakuwa na fursa ya kurefusha mkataba wa Pedro, 32, kwa miezi 12 zaidi mwishoni mwa msimu wa 2022-23.

Kandarasi ya Pedro na Chelsea ilitarajiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa Mei 2020 ila akarefusha zaidi mwanzoni mwa Juni hadi mwisho wa kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Kuondoka kwa Pedro kutatamatisha kipindi cha miaka mitano ya kuhudumu kwake kambini mwa Chelsea tangu atue jijini London, Uingereza mnamo Agosti 2015 baada ya kuagana rasmi na Barcelona waliompokeza malezi ya soka akiwa mtoto.

Hadi kufikia sasa, Pedro amewafungia Chelsea jumla ya mabao 43 kutokana na mechi 201 na aliwasaidia waajiri wake hao kunyanyua ubingwa wa EPL mnamo 2017, Kombe la FA mnamo 2018 na taji la Europa League mnamo 2019.

Tangu ujio wa kocha Frank Lampard kambini mwa Chelsea mwishoni mwa msimu jana, Pedro amewajibishwa mara 18 pekee katika mapambano yote. Hata hivyo, anatarajia kuwa sehemu ya kikosi kitakachosaidia Chelsea kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao na kutetea kwa mafanikio ufalme wa Kombe la FA muhula huu kabla ya kuondoka rasmi.

Katika juhudi za kujaza pengo la Pedro, Chelsea tayari wamejinasia huduma za Hakim Ziyech kutoka Ajax ya Uholanzi na Timo Werner kutoka RB Leipzig nchini Ujerumani. Wawili hao wanatazamiwa kutua rasmi uwanjani Stamford Bridge mwishoni mwa msimu huu.