• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
COVID-19: Visa 120 vipya, wagonjwa 42 wapona na mmoja afariki

COVID-19: Visa 120 vipya, wagonjwa 42 wapona na mmoja afariki

Na CHARLES WASONGA

WATU 120 zaidi wamepatikana na ugonjwa wa Covid-19 nchini Kenya na kufikisha 6,190 idadi jumla ya maambukizi.

Wagonjwa hao wa hivi punde wamepatikana baada ya sampuli 2,221 kupimwa ndani ya muda wa saa 24 zilizopita.

Kulingana na Waziri Msaidizi wa Afya Dkt Rashid Aman 115 miongoni mwao ni Wakenya huku watano wakiwa raia wa kigeni.

“Na Nairobi bado inaongoza kwa kuandikisha visa vingi vipya vya maambukizi ikifuatwa na Mombasa kisha Busia inashikilia nambari tatu kwa kuwa iko eneo la mpakani,” Dkt Aman amewaambia wanahabari Jumatatu katika makao makuu ya wizara hiyo jijini Nairobi.

Nairobi imeandikisha visa 64 vipya vya maambukizi, Mombasa (17), Kajiado (9), Machakos (9), Kiambu (8), Uasin Gishu (6), Nakuru (2) na Narok (2).

Dkt Aman ametangaza kuwa mtu mmoja amefariki kutokana na ugonjwa huo wa Covid-19 ndani ya muda wa saa 24 hivyo kufikisha 144 idadi ya watu ambao wameangamia tangu kisa cha kwanza cha ugonjwa huo kuripotiwa nchini.

“Mgonjwa huyu mmoja ni mwanamume aliyekuwa na umri wa miaka 69 wakati wa kifo chake na mkazi wa Mombasa ambaye alikuwa akiugua ugonjwa wa kisukari,” ameeleza Dkt Aman.

Waziri huyo msaidizi pia ametoa habari njema kwamba jumla ya wagonjwa 42 wamepona na kuruhusiwa kwenda nyumbani katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

“Kwa hivyo kufikia leo Jumatatu idadi jumla ya wagonjwa waliopona imepanda hadi kufika 2,013. Hii ni kutokana na kazi nzuri inayotekelezwa na wahudumu wetu wa afya,” Dkt Aman akaeleza.

You can share this post!

Mario Gomez astaafu baada ya kuisaidia VfB Stuttgart...

Waziri Amina amtakia Kamworor afueni baada ya kugongwa na...

adminleo