• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 3:25 PM
Mawakili wa Ngilu wavamiwa bunge la kaunti

Mawakili wa Ngilu wavamiwa bunge la kaunti

Na KITAVI MUTUA

MAWAKILI watatu wa Gavana wa Kitui Charity Ngilu, Jumatatu walishambuliwa na kutimuliwa kutoka majengo ya bunge la kaunti huku uhasama kati yake na madiwani ukichacha.

Mawakili hao, Bw Martin Oloo, Morris Kimuli na Stanley Kiima walikuwa wameenda katika bunge la kaunti baada ya madiwani kumwalika Bi Ngilu kufika mbele yao kuhusu madai ya sakata za utumizi mbaya wa mamlaka na fedha za umma.

Kizaazaa kilianza wakati mawakili hao walipoingia katika uwanja wa bunge la kaunti na kusimamishwa na walinzi wakielekea kwenye ofisi ya Spika George Ndotto.

Bw Ndotto alipowaona wakielekea ofisi yake aliwaagiza walinzi kuwafurusha.

Walinzi waliwavamia mawakili hao na wakamjeruhi Bw Kimuli mgongoni wakitekeleza amri ya Bw Ndotto. Mawakili hao walipiga ripoti katika kituo cha polisi cha Kitui.

Barua ya kumwalika Gavana Ngilu iliyoandikwa Juni 23, ilimweleza kwamba afike mwenyewe bungeni au akitaka angewakilishwa na mawakili wake kujibu madai yaliyo katika mswada unaolenga kumuondoa mamlakani.

Kwa kuwa bunge ilizimwa kumuondoa ofisini kufuatia agizo la mahakama na Spika hakuondoa barua ya kumwalika, Gavana Ngilu alituma mawakili wake kulalamika kwa Bw Ndotto.

Kwenye barua kwa Spika, Bi Ngilu kupitia mawakili wake, alimlaumu Bw Ndotto na karani wa bunge la kaunti, Bw Elijah Mutambuki kwa ubaguzi wa wazi katika mswada wa kumwondoa ofisini.

“Unaonekana kuwa na hujuma dhidi ya gavana,” ilisema barua ya mawakili hao.

Bi Ngilu alilaani shambulio dhidi ya mawakili wake na akamlaumu Bw Ndotto kwa kumpiga vita.

“Iwapo huu ni mswada halali wa kuniondoa, kwa nini wanatumia ukatili bila aibu kwa mawakili wangu?” alisema Gavana Ngilu.

You can share this post!

Chama cha ANC chalaumu siasa za Uhuru, Raila kufuatia...

UDAKU: Rebekah Vardy kukimbilia mahakama kutafuta haki...

adminleo