Bei ya unga kushuka
Na CHARLES WASONGA
NI rasmi sasa kwamba bei ya unga wa mahindi na ngano itashuka na hivyo kuwanusuru Wakenya kutokana na makali ya Covid-19.
Hii ni baada ya Rais Uhuru Kenyatta Jumanne jioni kutia saini bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2020/2021 na Mswada wa Fedha wa 2020 ambao umeondoa ushuru wa thamani ya ziada (VAT) ambao hutozwa bidhaa hizi za vyakula.
Wiki jana wabunge walipitisha marekebisho kadhaa ambayo yalipendekezwa na Kamati ya Fedha kwa Mswada huo ambao uliwasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha Ukur Yatani Aprili 2020.
Vilevile, wazee ambao hupokea pensheni kila mwezi wamepata afueni baada ya marekebisho yaliyofanyiwa mswada huo na kamati hiyo kupitishwa.
Wabunge waliondoa pendekezo la Waziri Yatani kwamba malipo ya pensheni yatozwe ushuru wa mapato kiasi cha asilimia 25 sawa na wafanyakazi ambao wangali kazini.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Joseph Limo (Mbunge wa Kipkelion Mashariki) aliwaongoza wabunge kupinga pendekezo hilo akidai hatua hiyo ni sawa na kuwatoza wazee hao ushuru maradufu.
“Wazee kama hawa ni watu ambao walikuwa wakilipa ushuru kwa miaka yote walipokuwa wakifanya kazi. Sasa kuanza kuwatoza ushuru kwa mara nyingine kutawaumiza zaidi na hii itakuwa sawa na wao kulipa ushuru mara mbili,” akasema Limo.
Kwa kuutia saini mswada huo, Rais Kenyatta pia aliidhinisha pendekezo la wabunge kwamba mpango wa kutoza gesi ya kupikia ushuru wa VAT wa kiasi cha asilimia 14 ucheleweshwe kwa muda wa mwaka mmoja.
Hii ni afueni kwa Wakenya, hasa wanaoishi katika maeneo ya mijini ambao hutumia gesi kupikia.
Rais Kenyatta pia alitia saini bajeti ya ziada ya mwaka wa kifedha wa 2019/2020 ambapo wabunge waliidhinisha Sh18.4 bilioni zitumike katika kushughulikia changamoto za kiafya zilizosababishwa na janga la Covid-19 kati ya masuala mengine ibuka.
Bajeti hiyo ya ziada na tatu katika mwaka wa kifedha uliokamilika Juni 30, 2020, pia inajumuisha Sh5 bilioni zilizotengewa serikali za kaunti kufadhili mipango ya kukabiliana na janga la Covid-19.
Aidha, zilijumuisha Sh3.4 bilioni zilizotengewa mpango wa kuwapa marupurupu maalum wahudumu wa afya walioko mstari wa mbele kukabiliana na janga hilo.
Hafla hiyo fupi ya kutiwa saini kwa miswada hiyo ilifanyika katika Ikulu ya Nairobi na kuhudhuriwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, Waziri Yatani na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Amos Kimunya.
Wengine walikuwa Wakili Mkuu wa Serikali Kennedy Ogeto, Karani wa Bunge la Kitaifa Michael Sialai na Naibu Mkuu wa Wafanyakazi katika Ikulu Njee Muturi.