Kimataifa

Burundi yakiri Covid-19 ni hatari

July 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na AFP

GITEGA, BURUNDI

RAIS mpya wa Burundi, Evariste Ndayishimiye sasa ametangaza virusi vya corona kuwa “adui mkuu” anayelikabili taifa hilo.

Tangazo lake ni kinyume na mwelekeo wa awali nchini humo, ambapo uwepo wa virusi hivyo haujakuwa ukichukuliwa kwa uzito.

Rais Ndayishimiye na mtangulizi wake, Pierre Nkurunziza aliyefariki Juni 2020, walikuwa wakipuuzilia mbali athari za virusi hivyo.

Walikuwa wakishikilia kuwa Mungu ameiepushia nchi hiyo janga hilo.

Burundi iliendesha kampeni za uchaguzi mkuu wa Mei kama kawaida, licha ya majirani wake kuweka mikakati thabiti kukabili maambukizi ya virusi.

Kulingana na takwimu rasmi zilizotolewa na serikali, taifa hilo limethibitisha visa 170 na kifo kimoja pekee kwa muda wa miezi miwili.

Rais Ndayishimiye alikuwa akizungumza mnamo Jumanne, muda mfupi baada ya kuiapisha serikali yake mpya katika majengo ya Bunge.

“Kuanzia kesho (juzi Jumatano), nimetangaza virusi vya corona kuwa tishio kubwa zaidi linalowakumba raia wa Burundi. Hii ni kwa kuwa vimeibua hofu kubwa miongoni mwao. Tumejitolea vilivyo kukabili janga hili,” akasema.

Aliwaomba raia “kuzingatia kanuni za kudhibiti maambukizi yake ambazo zitatolewa na Wizara ya Afya kote nchini humu.”

Alisema kuwa ili kuongeza kiwango cha usafi miongoni mwa raia wake, serikali itapunguza bei ya sabuni kwa asilimia 50 na hata gharama ya maji.

Aliwaambia raia kuwa hawatatozwa malipo yoyote kupimwa ikiwa wameambukizwa na kutibiwa.

Aliwaonya wale ambao hawakujitokeza kupimwa wakati walionyesha dalili za virusi kufanya hivyo mara moja.

“Katika siku zijazo, ikiwa mtu hataenda kupimwa, itaonyesha kuwa lengo lake ni kuwaambukiza wengine kimakusudi. Atachukuliwa kama adui wetu na kukabiliwa vikali kisheria,” akasema.

Kufika sasa, taifa hilo lina kituo kimoja pekee cha kuwapima watu ikiwa ama wameambukizwa au la.

Zaidi ya hayo, kituo hicho kina wahudumu chini ya 10

Hata hivyo, kiongozi huyo aliahidi kuongeza vituo zaidi vya kuwachunguza watu kote nchini humo.

“Tutazindua kampeni kuwapima watu katika maeneo ambako virusi vitabainika kuwepo kwa wingi. Lazima adui akabiliwe kwa njia zote, hata kwenye maeneo ambako amejificha,” akaeleza.

Kwa hayo, aliwaomba wahudumu wa afya, viongozi wa kidini na wanahabari kuwashinikiza watu kuzingatia kanuni za kusaidia kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo vya corona.

“Lazima kila mmoja afahamu kuwa virusi hivi ni janga hatari ambalo linasambazwa kwa urahisi na kumwathiri aliyeambukizwa kwa wakati mfupi sana,” akasema.

Afisa mmoja wa ngazi za juu katika Wizara ya Afya, alisema kuwa hatua ya serikali kuchukua mwelekeo huo mpya unatokana na Benki ya Dunia kutoa Sh500 milioni mwezi uliopita kuisaidia kuendesha juhudi za kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo.