Magoha amrushia Uhuru kiazi moto cha kufungua shule
Na FAITH NYAMAI
UAMUZI kuhusu lini shule zitakapofunguliwa, sasa umo mikononi mwa Rais Uhuru Kenyatta.
Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, Jumatano alisema kutokana na mashauriano na wataalamu wa afya, imetambuliwa kuna uwezekano mkubwa idadi ya watu wanaoambukizwa corona itafikia upeo wake Septemba.
Rais alikuwa ameambia Wizara ya Elimu kwa ushirikiano na idara nyingine zinazoshiriki katika juhudi za kupambana na virusi vya corona, watafute jinsi watoto wanavyoweza kurudi shuleni kuanzia Septemba.
Jana, Waziri Msaidizi wa Afya, Dkt Rashid Aman alitangaza idadi kubwa zaidi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa kwa siku moja.
Watu 307 walipatikana na virusi hivyo na kufikisha idadi ya wagonjwa hadi 6,673.
Idadi ya waliopona ilifika 2,089 baada ya wagonjwa 50 kuruhusiwa kwenda nyumbani. Hata hivyo, idadi ya waliofariki ilifika 149 baada ya mgonjwa mwingine kufariki dunia.
Kwa kuzingatia takwimu za sasa, Prof Magoha alisema itakuwa vigumu kuamua shule zote zifunguliwe Septemba kwani imetabiriwa maambukizi yataanza kupungua Januari mwaka ujao.
“Kuna maelewano tumefanya na hilo litatangazwa na yule anayesimamia mikakati yote (Rais) kwa hivyo tusubiri hadi atakapohutubia nchi,” akasema.
“Mnamo Jumatatu, Julai 6, 2020, Rais Uhuru Kenyatta atatoa tangazo rasmi kuhusu ni lini shule zitafunguliwa,” aliongeza waziri Magoha.
Akizungumza wakati wa mkutano na viongozi wa vyama vya wafanyakazi wa sekta ya elimu katika taasisi ya ukuzaji wa mitaala (KICD), Profesa Magoha alisema wizara haitaweka afya ya wanafunzi hatarini.
Alisema msimamo wa wadau, wakiwemo wazazi na magavana ni kwamba, shule hazifai kufunguliwa hadi maambukizi yatapoanza kupungua.
Mkutano wa jana ulihudhuriwa na maafisa wa vyama vya walimu vya Knut na Kuppet. Chama cha wahadhiri wa vyuo vikuu (Uasu), chama cha walimu wwanawake (Kewota), chama cha walimu wakuu wa shule za sekondari (Kessha) na chama cha walimu wakuu wa shule za msingi (Kepsha) miongoni mwa vingine.
Mjadala kuhusu ni lini shule zinafaa kufunguliwa umekuwa ukiendelea tangu Juni.
Mitihani ya kitaifa tayari imeahirishwa hadi Aprili 2021.
Rais Kenyatta alikuwa ameagiza wizara ya elimu kufanya maandalizi ya shule kufunguliwa Septemba. Kama sehemu ya maandalizi, Profesa Magoha alisema shule zitapatiwa maski 24 milioni zitakazogawiwa wanafunzi.
Waziri Magoha pia amesema kila shule itakuwa na matangi ya maji kuwezesha wanafunzi kunawa mikono mara kwa mara.