• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 12:46 PM
COVID-19: Visa jumla vyakaribia 7,000

COVID-19: Visa jumla vyakaribia 7,000

Na SAMMY WAWERU

VISA vipya 268 kutoka kwa sampuli 2,704 katika muda wa saa 24 zilizopita vimefikisha 6,941 idadi jumla nchini.

Waziri Msaidizi katika Wizara ya Afya Dkt Rashid Aman amesema Alhamisi kwamba kufikia sasa, Kenya imekagua takriban sampuli 176,059

Kati ya visa vipya vya Alhamisi, wagonjwa 259 ni Wakenya huku tisa wakiwa raia wa kigeni.

“Katika maambukizi haya mapya, 160 ni jinsia ya kiume, kike wakiwa 108,” Dkt Aman amewambia wanahabari katika Afya House jijini Nairobi.

Aidha, amesema mgonjwa wa umri wa chini ni mtoto wa mwaka mmoja, umri wa juu miaka 80.

Kaunti ya Nairobi imeandikisha idadi ya juu ya maambukizi 175, Mombasa (28), Busia (18), Kiambu 11, Kajiado na Migori visa 9 kila moja.

Uasin Gishu imeandikisha wagonjwa wanane, Machakos (6), Narok (2), huku Makueni na Murang’a kisa kimoja kila kaunti.

Imekuwa afueni baada ya wagonjwa 20 kuruhusiwa kuondoka katika vituo vya afya walivyokuwa wakipokea matibabu baada ya kuthibitishwa kupona kabisa. Idadi jumla ya waliopona nchini sasa imefika 2,109.

Dkt Aman pia amethibitisha wagonjwa watatu wamefariki kutokana na corona katika kipindi cha saa 24 zilizopita, idadi jumla ya waliofariki nchini ikigonga 152.

Ameshauri Wakenya na wakazi wengine nchini kuzingatia masharti na kanuni za kuepuka maambukizi.

Ameongeza kwamba Kenya ingali na kibarua kigumu kuhakikisha visa vya maambukizi ya vinarudi chini.

Dkt Aman hata hivyo amesema kasi ya maambukizi ya ugonjwa huu unaosababishwa na virusi vya corona itadhibitiwa ikiwa kila mwananchi atatii na kutilia mkazo sheria na mikakati iliyowekwa.

“Ninawakumbusha kibarua tulichonacho ni kigumu, ila hatuko mbali kudhibiti hali kwa kuzingatia mikakati tuliyoweka,” akasema.

You can share this post!

Wanafunzi kutoka Sudan wapimwa

Alexis Sanchez na Ashley Young wasaidia Inter Milan...

adminleo