Upatanisho wa Waiguru na MCAs watatizika
GEORGE MUNENE na KENNEDY KIMANTHI
JUHUDI za kupatanisha Gavana Anne Waiguru na wawakilishi wa Bunge la Kaunti ya Kirinyaga zilipata pigo jana, baada ya MCAs kukataa jopo linalodaiwa kubuniwa kwa ajili ya kuwaleta pamoja.
Mmoja wa wanaosemekana kuteuliwa kwenye jopo hilo la watu saba, Askofu Mkuu Anthony Muheria wa Dayosisi ya Nyeri ya Kanisa Katoliki, alisema hakuwa na habari ya kuwepo kwa jopo hilo.
“Hakuna yeyote aliyewasiliana nami kunijulisha kuhusu jambo hilo. Sijafahamishwa na gavana. Nitasubiri nione kama atanipigia kunijulisha kuhusu jopo hilo,” Askofu Muheria akaambia Taifa Leo kwa njia ya simu.
Ijumaa, gavana Waiguru alitoa taarifa iliyoeleza kuhusu kubuniwa kwa jopo la watu saba, akidai watakuwa na jukumu la kumpatanisha yeye na mahasimu wake wa kisiasa.
Mbali na Askofu Mkuu Muheria, wengine ni Makatibu wa Wizara Paul Maringa (Miundomsingi), Nancy Karigithu (Bahari), Mary Kimonye (Huduma za Umma, Vijana na Jinsia) na aliyekuwa Katibu Mkuu, Bw J.S Mathenge.
Wengine ni John Njiraini (Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa KRA) na Bw Charles Ndegwa, ambaye ni pasta kutoka eneo la Mwea.
Pasta Ndegwa wa kanisa la Jesus is Lord for All Church, pia alisema hakuwa amefahamishwa kuhusu kuteuliwa kwake kwenye jopo hilo. Hata hivyo, alisema yupo tayari kushiriki kwenye upatanishi huo kwa manufaa ya wakazi wa kaunti yake.
“Ni wazo zuri, japo sijafahamishwa na wala sina habari kwa sasa. Nimesikia sasa kwamba jina langu limetajwa lakini sijapigiwa simu wala kuandikiwa ujumbe. Nataka niseme kuwa niko tayari kushiriki katika kurejesha utulivu katika uongozi wa kaunti. Uhusiano huo mbaya kati ya gavana na MCAs unarejesha nyuma maendeleo ya Kirinyaga,” akasema.
Gavana Waiguru na sehemu kubwa ya MCAs wa Kirinyaga waliojaribu kumtimua kazini, wamekuwa hawasikizani.
MCAs wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi, Bw Kamau Murango walisisitiza kutoshiriki kwenye mazungumzo hayo ya upatanisho.
Wiki jana, Bi Waiguru alinusuriwa na Bunge la Seneti, baada ya kamati ya watu 11 iliyoongozwa na Seneta wa Kakamega, Cleophas Malala kusema hakuwa na makosa. Gavana kwenye ujumbe wake jana, alisema walioteuliwa kuleta mapatano ni watu wasioegemea mirengo ya kisiasa na kwamba wanatoka eneo hilo.
Bi Waiguru hakupatikana ili kumfichua aliyependekeza majina hayo, na kwa nini alifahamu yeye kwanza kabla ya walioteuliwa.