• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
WHO yakana China ilitangulia kuifahamisha kuhusu corona

WHO yakana China ilitangulia kuifahamisha kuhusu corona

Na AFP

SHIRIKA la Afya Ulimwenguni (WHO) limebadili kauli yake ya awali kwamba China ndio ililipasha habari kuhusu mlipuko wa janga la Covid-19 jijini Wuhan katika Mkoa wa Hubei.

Shirika hilo sasa linasema lilipata habari kutoka afisi yake iliyoko China.

WHO imekuwa ikilaumiwa na Rais wa Amerika Donald Trump kwa kufeli kutoa habari sahihi kusaidia kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo na kwamba imekuwa ikiitetea China, madai ambayo shirika hilo lilikana.

Ni tuhuma hizo zilizopelekea Rais Trump kuzima misaada ambayo Amerika imekuwa ikitoa kwa WHO.

Mnamo Aprili 9, 2020, WHO ilichapisha msururu wa habari taarifa ilizotoa baada ya kuripotiwa kwa mkurupuko wa virusi vya corona nchini China mwishoni mwa mwaka 2019.

Hii ni baada ya Amerika kuikosoa kwamba ilifeli kutoa habari sahihi kuhusu chimbuko la janga hilo ambalo kufikia sasa limesababisha vifo vya zaidi ya watu 521,000 ulimwenguni.

Katika taarifa hiyo, WHO ilisema kwamba tume ya afya jijini Wuhan katika mkoa wa Hubei mnamo Desemba 31, 2019 iliripoti visa vya homa hiyo. Hata hivyo, shirika hilo halikufichua ni wapi lilipata habari hizo.

Akihutubia kikao cha wanahabari mnamo Aprili 20 Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedro Adhanom Ghebreyesus alisema kuwa ripoti ya kwanza kuhusu mlipuko wa virusi vya corona ilitoka China.

Hata hivyo, hakufafanua ikiwa habari hizo zilitumwa na maafisa wa China au walizipata kwingineko.

Lakini katika taarifa mpya iliyochapishwa na WHO wiki hii inatoa ufafanuzi zaidi kuhusu habari za kwanza kuhusu Covid-19.

Shirika hilo linaeleza kuwa ni afisi yake nchini China ambayo mnamo Desemba 31 iliwapasha maafisa wake kuhusu kisa cha kwanza cha homa hiyo. Hii ni baada ya kupata habari hizo kutoka kwa tovuti ya tume ya afya jijini Wuhan.

Siku hiyo, kitengo cha WHO cha magonjwa ya kuambukiza kilipata habari zingine zilizotolewa na shirikia la kuchunguza milipuko ya magonjwa kwa jina, ProMed. Shirika hilo lenye makao yake Amerika pia liliripoti kuhusu visa vya homa hiyo hiyo jijini Wuhan.

Ni baada ya hapo ambapo WHO iliitisha maelezo zaidi kuhusu visa hivyo vya maambukizi ya virusi vya corona, na ikapewa taarifa hizo mnamo Januari 3.

Mkurugenzi wa WHO anayesimamia kitengo cha magonjwa ya kuambukiza Michael Ryan Ijumaa aliwaambia wanahabari kwamba shirika hilo huzipa nchi muda wa hadi saa 48 kuthibitisha kisa cha mlipuko wa magonjwa na kuipa asasi hiyo maelezo kuhusu chanzo chake.

Rais Trump aliikashifu WHO kwa usimamizi mbaya wa habari kuhusu janga hilo huku akidai shirika hilo la Umoja wa Mataifa (UN) ni “kibaraka” cha China.

You can share this post!

JAMVI: Ndiye mrithi wa Uhuru Mlimani?

Mbadi akanusha mzozo bungeni kati ya ODM, Jubilee kuhusu BBI

adminleo