ONYANGO: Vyama vya kisiasa havifai kufadhiliwa kwa pesa za umma
Na LEONARD ONYANGO
KUNA haja ya kubadili Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2011 ili kuondoa kifungu kinachotaka viwe vikifadhiliwa na fedha za walipa ushuru.
Kulingana na sheria hiyo, vyama vinavyopata angalau asilimia tano ya jumla ya kura zilizopigwa katika Uchaguzi Mkuu vinafuzu kupokea mgao wa fedha hizo.
Sheria hiyo inataka asilimia 0.3 ya mapato ya nchi kutengewa vyama vya kisiasa.
Jumla ya kura huzingatia idadi ya kura ambazo wawaniaji wa chama husika wanapata katika kinyang’anyiro cha urais, magavana, wabunge na wawakilishi wa wadi.
Mathalani, katika uchaguzi mkuu wa 2017, vyama viwili tu; Jubilee na ODM, vilitimiza vigezo vinavyohitajika ili kunufaika na fedha hizo.
Vyama vidogo vimekuwa vikishinikiza sheria hiyo ifanyiwe mabadiliko ili fedha hizo zigawanywe kwa usawa miongoni mwa vyama vyote vilivyosajiliwa.
Mwaka jana, Wizara ya Fedha ililalamika kuwa kiasi cha fedha zinazofaa kutengewa vyama vya kisiasa ni cha juu zaidi na kuahidi itawasilisha mswada unaolenga kufanyia mabadiliko sheria hiyo.
Wizara ya Fedha ilisema kuwa imekuwa ikitenga Sh371 milioni kwa ajili ya vyama vya kisiasa tangu 2015 badala ya Sh3.6 bilioni zinazofaa kutolewa kulingana na Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2011. Wizara ilielezea kuwa imekuwa ikitoa kiasi cha chini cha fedha kwa vyama vya kisiasa kutokana na fedha za kutosha.
Lengo la sheria hiyo kutengea vyama vya kisiasa fedha lilikuwa kuimarisha demokrasia vyamani na nchini.
Lakini ukweli ni kwamba misukosuko ambayo tumekuwa tukishuhudia hivi karibuni katika vyama vya kisiasa ni ithibati tosha kwamba vyama ni mali ya watu binafsi na havifai kufadhiliwa na fedha za walipa ushuru.
Vyama vya kisiasa vya humu nchini haviongozwi na sera bali vinatumiwa kunufaisha wachache.
Mathalani, kauli iliyotolewa hivi karibuni na mbunge wa Suna Mashariki kuwa wanasiasa wa ODM wanafuata kinara wao Raila Odinga kama ng’ombe, ni ithibati tosha kwamba chama hicho ni mali ya mtu binafsi.
Chama cha ODM pia kimekataa kugawana fedha hizo na vyama vingine vya muungano wa NASA vilivyounga mkono Bw Odinga katika uchaguzi mkuu wa 2017.
Msukusuko unaokumba Jubilee pia umedhihirisha kuwa hakuna demokrasia ndani ya chama hicho. Rais Kenyatta amekuwa akiwaadhibu wandani wa Naibu wa Rais William Ruto wanaokosoa namna chama hicho kinavyoendeshwa.
Hivyo, hakuna haja ya kutumia ya mamilioni ya fedha za walipa ushuru kufadhili vyama vya kisiasa.