• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
WANGARI: Kenya isitoze kodi tasnia za kidijitali ili kuinua biashara

WANGARI: Kenya isitoze kodi tasnia za kidijitali ili kuinua biashara

Na MARY WANGARI

HUKU biashara na mashirika mbalimbali yakikumbatia mifumo ya kidijitali katika utekelezaji wa shughuli zao kutokana na athari za Covid-19, ni bayana mjadala kuhusu Kodi ya Huduma za Kidijitali (DST), hauwezi ukaendelea kupuuzwa.

Tayari kuna Mswada wa Fedha 2020, unaopendekeza kutoza DST dhidi ya mapato kutokana na tasnia za kidijitali kwa kiwango cha asilimia 1.5 cha thamani ya mapato ya jumla.

Iwapo itatekelezwa, hatua hiyo inatazamiwa kuathiri tasnia za kidijitali ikiwemo: mitandao ya maelezo kama vile google, mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, Instagram na kadhalika.

Mitandao ya kuchapishia na kutazama video, michezo na matangazo kidijitali na shughuli nyinginezo zinazofanyika kupitia mitandao ya kijamii, ni miongoni mwa shughuli zinatotarajiwa kujumuishwa katika DST.

Japo hatua hiyo ya kutoza kodi huduma za kidijitali ilidhamiriwa kuongeza mapato kutokana na ushuru unaokusanywa kwa kujumuisha uchumi kidijitali, bado kuna changamoto zinazopaswa kushughulikiwa ili kufanikisha mchakato huo.

Akitoa hotuba ya Bajeti 2019, Waziri wa Fedha Ukur Yatani alitaja baadhi ya changamoto hizo zinazohusiana na uchumi kidijitali kama vile: matumizi ya kiasi kikubwa cha data, mifumo anuai ya kibiashara, udhahania na kadhalika.

Hatua ya utozaji kodi biashara za kidijitali tayari imeshughulikiwa katika Sheria ya Kodi kuhusu Mapato Kenya, inayofafanua soko la kidijitali kama: tasnia inayowezesha mtagusano wa moja kwa moja kati ya wanunuzi na wauzaji bidhaa na huduma kupitia mfumo wa kielektroniki.

Hata hivyo, pana haja ya kubuniwa sheria mwafaka zitakazowezesha utekelezaji ufaao wa ushuru kuhusu mapato ya kidijitali ili kuondoa utata kati ya biashara kidijitali na biashara kielektroniki.

Isitoshe, ikizingatiwa kuwa kodi hiyo inajikita katika thamani ya jumla ya mapato, pana haja ya kuainisha waziwazi huduma zitakazojumuishwa katika DST.

Sababu ni kwamba, sheria ya sasa ni pana ilhali mashirika mengi yanajumuisha kijisehemu cha biashara zinazofanyika kielektroniki.

Ni bayana hatua ya kushirikisha umma kuhusu sheria ya ushuru wa huduma kidijitali mwezi uliopita, ilitoa fursa kwa wadau kutoa mapendekezo yao.

Hata hivyo, bado kuna mwendo mrefu ikizingatiwa kutoza ushuru soko la kidijitali bado ni suala linalozingirwa na utata kimataifa.

Aidha, mataifa ya Magharibi yakiongozwa na Amerika yamekuwa yakipinga DST na ni dhahiri kuanza kutekeleza hatua hiyo, ni sawa na kuanzisha vita vya kibiashara na mataifa hayo makubwa.

You can share this post!

WASONGA: Itakuwa kibarua sasa kwa kaunti kuzuia maambukizi...

Asukumwa jela kwa kuiba kuku

adminleo