• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 1:50 PM
Masharti makali kwa wanaotaka kwenda mashambani

Masharti makali kwa wanaotaka kwenda mashambani

Na WAANDISHI WETU

WAKAZI wa sehemu za miji wanaopanga kurudi nyumbani maeneo ya mashambani baada ya vikwazo vya usafiri kuondolewa Nairobi na Mombasa, watahitajika kutimiza masharti makali ambayo yanaendela kuwekwa na magavana.

Magavana na makamishna wa kaunti za Nyanza na Magharibi wameshirikiana kuzuia usambazaji wa virusi vya corona eneo hilo wanapotarajia kupokea idadi kubwa ya watu hivi karibuni.

Kufikia jana, usafiri ulikuwa ungali haujashika kasi kwani wamiliki wa mabasi ya uchukuzi wa umma hawajapata vibali vipya vinavyohitajika.

Kando na kukaguliwa ikiwa wana dalili za maambukizi ya corona kabla kuingia kaunti hizo, watahitajika kujitenga kivyao kwa siku 14 kabla waruhusiwe kutangamana na wengine katika jamii.

Kamshna wa eneo la Magharibi, Bi Anne Ngetich jana alisema kampeni ya uhamasisho inaendelezwa kwa wenyeji mashambani ili wasaidie kudhibiti maambukizi watakapopokea wageni.

Alisema tayari maafisa wameagizwa kushika doria katika mipaka ya kaunti barabarani kuhakikisha hakuna yeyote atakayekiuka masharti.

“Ingawa ni muhimu kuwa wabaki katika maeneo yenye idadi kubwa ya maambukizi hadi yadhibitiwe, hatuwezi kuwazuia wale wanataka kuja nyumbani. Lakini tunawaomba kujitenga wanapowasili nyumbani, na wale wengine waendelee kuzingatia masharti ya wizara ya afya,” akasema Bi Ngetich.

Mnamo Jumatatu, Rais Uhuru Kenyatta aliondoa marufuku ya kuingia na kuondoka kaunti za Nairobi, Mombasa na Mandera.

Alisema sasa itakuwa ni wajibu wa kila mwananchi kujikinga dhidi ya maambukizi kwa kufuata kanuni zilizowekwa kama vile kuvalia barakoa, kunawa mikono kila mara na kutotangamana na wengine.

Katika kaunti ya Kisumu, Gavana Anyang’ Nyong’o alisema maafisa wake kwa ushirikiano na wale wa usalama wameimarisha ukaguzi katika maeneo ya mpaka na viingilio vingine katika kaunti hiyo.

“Maafisa wetu walioko katika sehemu hizo wanahakikisha kuwa wale wote wanaongia Kisumu wanashuka na maelezo yao kuchukuliwa na kupimwa joto. Hii itahakikisha wanaoelekea vijijini hawapeleki ugonjwa huo kwa wazee,” akasema.

Katika kaunti ya Siaya, Gavana Cornel Rasanga alisema wale wanaowasili kutoka Nairobi na Mombasa watakaguliwa katika vituo maalum saba ambavyo vimetengwa.

“Baada ya kuchunguzwa na kupimwa joto, watapewa barakoa mpya na kuhimizwa kufuata masharti ya Wizara ya Afya,” akasema Bw Rasanga, kauli ambayo pia iliungwa mkono na Kamishna wa Kaunti ya Siaya, Michael Ole Tialal.

Katika kaunti ya Homa Bay, Kamishna wa Kaunti Yatich Kipkemei aliwataka wakazi kuchukua wajibu wa kibinafsi kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona vijijini.

Naye kamishna wa Kaunti ya Vihiga, Bw Ochilloh Oyugi alisema watu wote watakaopimwa joto na kupatikana dalili zozote watatengwa katika Chuo Anua cha Keveye kwa siku 14.W

aziri wa Uchukuzi James Macharia jana alisema, serikali tayari imeandaa kibali maalumu ambacho kila gari linaloenda mashambani kutoka kaunti zilizokuwa zimefungwa, litahitajika kuwa nacho kabla ya kurejelea huduma.

Waziri Macharia pia alitangaza kuwa huduma ya treni ya Madaraka Express kati ya Nairobi na Mombasa itaanza safari zake Jumatatu.

Treni hiyo ya SGR itakuwa na sehemu maalumu ya kutenga mtu yeyote ambaye ataonyesha dalili za Covid-19 akiwa safarini, kwa mujibu wa Bw Macharia.

Ripoti za Benson Amadala, Rushdie Oudia, Dickens Wasonga, George Odiwuor, Derrick Luvega na Charles Wasonga

You can share this post!

Familia yateta chifu kuagiza warudishe mahari

Masharti ya safari za ndege yalegezwa

adminleo