• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Majina ya wanakamati bungeni kuidhinishwa Jumanne

Majina ya wanakamati bungeni kuidhinishwa Jumanne

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Kitaifa litafanya kikao maalum Jumanne kuidhinisha majina wa wabunge waliopendekezwa kuhudumu katika nafasi zilizobaki katika kamati mbalimbali baada ya wandani wa Naibu Rais William Ruto kutimuliwa.

Hii ni baada ya mirengo ya  NASA na Jubilee kusuluhisha tofauti kati yao kuhusu kuhusu uteuzi wa wanachama wa kamati ya Haki na Masuala ya Sheria (JLAC) na Kamati kuhusu Sheria Mbadala (Delegated Legislation).

Kamati hizo mbili zitakuwa na wajibu mkubwa katika utayarishaji wa sheria zitatakazotumiwa kufanikisha utekelezaji wa mageuzi yatakayopendekezwa  kwenye ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI). Kamati hizo mbili pia mswada wa kura ya maamuzi na miswada mingine ya marekebisho ya katiba.

Hii ndio maana kiongozi wa wachache John Mbadi alipinga hatua ya kiongozi wa wengi Amos Kimunya kuteua idadi kubwa wa wabunge wa mrengo wa Tangatanga katika kamati ya JLAC kwa misingi wamekuwa wakipinga mpango wa BBI na muafaka kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Kwa mfano, Mbadi alipendekeza majina ya wabunge Gladys Shollei (Mbunge Mwakilishi wa Uasin Gishu), Gitonga Murugara (Tharaka) na John Kiarie (Dagoreti Kusini) ambao ni wandani wa Dkt Ruto waondolewa kutoka orodha ya wanachama wa JLAC.

Kulingana na Mbunge huyo wa Suba Kusini wabunge kama hao ambao wamekuwa wakipinga mpango wa BBI wanaweza kuhujumu mipango ya kupitishwa kwa ripoti hiyo ambayo inasubiri kuwasilishwa kwa Rais Kenyatta.

Hii ndio maana wiki jana, Bw Kimunya alilazimika kuondoa orodha ya wanachama wapya wa kamati hizo mbili ili kutoa nafasi kwa majadiliano na kupatikana kwa muafaka.

Hatimaye mnamo Jumatatu, Julai 6, 2020, Kimunya alikubalia kuondoa majina ya wabunge wa mrengo wa tangatanga kutoka orodha ya wanachama wa JLAC na kamati kuhusu Sheria Mbadala.

Katika mkutano uliohudhuriwa na kiranja wa wachache Junet Mohamed, ilikubaliwa pia kwamba upande wa wachache (Nasa) atapewa nafasi za uenyekiti wa kamati za Fedha na Elimu. Hii ni baada ya Bw Kimunya kukubali kujumuisha kuorodhesha wabunge wa Jubilee ambao wanaweza kuwachagua wabunge wa upinzani kuongoza kamati hizo.

“Nilifanya mkutano na Kiongozi wa Wengi kuhusu suala la uteuzi wa wanachama wa kamati za bunge. Tumekubaliana kuhusu orodha ambayo itawalishwa bungeni juma lijalo,” Juneti akasema.

Orodha hiyo mpya itaidhinishwa na Kamati kuhusu Uteuzi mnamo Jumatatu wiki ujao kabla ya kuwasilishwa bunge siku itakayofuata. Kamati hiyo yenye wanachama 19, akiwemo kiongozi wa wachache,  huongozwa na kiongozi wa wengi.

Wajibu mkuu wa Kamati hiyo ya Uteuzi huwa ni kuteua majina ya wabunge watakaohudumu katika kamati mbalimbali za bunge, isipokuwa Kamati ya Kuratibu Shughuli za Bunge na Kamati ya Kuwapiga Msasa watu waliopendekezwa kushikilia nyadhifa kuu serikalini.

Mbw Kimunya na Mbadi watawasilisha ombi kwa Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi ili aitishe kikao maalum cha bunge. Wabunge walioaliza likizo ya majuma matatu mnamo Jumatano wiki jana.

Ni katika kikao hicho ambapo ripoti ya Kamati ya Fedha iliyompiga msasa mteule wa wadhifa wa Mkaguzi Mkuu wa Matumizi ya Fedha za Serikali Nancy Janet Kabui Gathungu itajadiliwa na kupitishwa.

You can share this post!

Masharti ya safari za ndege yalegezwa

Ujenzi wa soko la kisasa Garissa wakaribia kukamilika

adminleo