Magavana wawili zaidi kuchunguzwa kwa ufisadi
Na CHARLES WASONGA
MAGAVANA wengine wawili watashtakiwa kwa kosa la ufisadi hivi karibuni huku Tume ya Madili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ikizidisha vita dhidi ya uovu huo.
Afisa Mkuu Mtandaji wa tume hiyo Twalib Mbarak alifichua habari hizo Alhamisi japo hakutaja majina ya magavana watakaokamatwa.
“Siwezi kukufichulia sasa majina yao, lakini hivi karibuni watajulikana. Kile ningependa kukuhakikisha kuwa tunawachunguza magavana kutoka mirengo yote ya kisiasa,” Bw Mbarak akaambia mtangazaji wa runinga ya Citizen, Yvonne Okwara, kwenye mahojiano Alhamisi usiku.
“Kile nataka Wakenya wafahamu ni kwamba baada ya mwezi mmoja au miezi miwili, magavana wengine wawili watafikishwa kortini. Wengi wao wanachunguzwa,” Bw Mbarak akasema.
“Niliahidi kuwaandama nyani wakubwa, pindi tu nilipoingia afisini. Kwa hivyo, kazi hiyo tunaifanya kwa uadilifu mkubwa,” akaongeza.
Kufikia sasa magavana wanaokabiliwa na kesi za ufisadi mahakamani ni Mike Sonko (Nairobi), Moses Lenolkulal (Samburu) na Sospeter Ojaamong’ (Busia).
Katika mahojiano hayo, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji alisema kesi kuhusu sakata ya mabwawa ya Arror na Kimwarer itachukua muda mrefu kukamilika.
“Hii ni kwa sababu ya masuala magumu yanayohusiana kesi hizo ikiwemo kutafuta usaidizi wa serikali za mataifa ya nje katika mchakato wa uchunguzi, kwani sakata hiyo ilihusu raia wa kigeni,” akasema Bw Haji.
Hata hivyo DPP alielezea matumaini kuwa kesi hizo zitakamilika baada ya miaka miwili
Bw Haji alikuwa akijibu swali kuhusu ni kwa nini kesi hizo zimechukua muda mrefu kukamilishwa.
Aliyekuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich na aliyekuwa Katibu katika Wizara hiyo Kamau Thugge ni miongoni mwa maafisa wakuu serikalini ambao walifunguliwa mashtaka kuhusiana na sakata hiyo iliyohusu kupotea kwa Sh21 bilioni.
Kuhuusu sakata ya ardhi ya Ruaraka, Bw Haji alipuuzilia mbali madai kuwa afisi yake inagopa kushughulikia kesi hiyo.
Alisema suala hilo tayari linashughulikiwa na mahakama ya rufaa kwa hivyo ipo haja ya kusubiri matokeo.
“Matokeo ya kesi hiyo yatatoa mwelekeo kuhusu hatua nyingine ambayo itachukuliwa kuhusiana na suala hilo. Uamuzi kuhusu iwapo wahusika watafunguliwa mashtaka itategemea uamuzi utakaotolewa na mahakama ya rufaa,” akasema Bw Haji.
Katika sakata hiyo inadaiwa kuwa Wizara ya Elimu ililipa Sh1.5 bilioni kama awamu ya kwanza ya fidia ya ardhi ya ukubwa wa ekari 96 ambako kumejengwa shule msingi ya Drive Inn na Shule ya upili ya Ruaraka.
Pesa hizo, ambazo zilikuwa sehemu ya Sh4.3 bilioni ambazo zilipaswaa kulipwa kampuni ya Afrison Import Export and Hueland inayomilikiwa na mfanyabiashara Francis Mburu.