Habari

Masharti ya kuzima wazee yazua kizuizi kwa ufunguzi wa makanisa

July 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

TITUS OMINDE, DIANA MUTHEU na MAUREEN ONGALA

IBADA ndani ya makanisa na misikiti huenda zikaathirika, baada ya viongozi wa kidini kusema mojawapo ya masharti ya ufunguzi inawazuia wao kushiriki.

Kwenye kikao na wanahabari mjini Eldoret, Jumapili, viongozi hao walisema sharti la kuzuia watu wa zaidi ya miaka 58 linawazuia wengi wao kushiriki ibada hizo.

“Sharti la kuzuia wazee wa umri wa miaka zaidi ya 58 kuhudhuria ibada ni pigo kwa kanisa. Makanisa yetu mengi yanaongozwa na wazee. Vijana wamepotelea katika pombe na hawana ufahamu wa mambo ya dini,” akasema kiongozi wa muungano huo wa waumini, Askofu Wilson Kirui.

Walidai vikwazo vilivyowekwa vina nia fiche ya kulemaza kanisa, hivyo basi hawakubaliani na kamati iliyohusika kutoa mapendekezo hayo kwa Rais Uhuru Kenyatta.

“Kuzuia wazee kuhudhuria ibada ni sawa na kuacha kondoo bila mchungaji,” akasema Askofu Kirui.

Naye Kasisi Boniface Simani wa kanisa la Bread Of Life, aliitaka serikali iondoe vikwazo hivyo, akisema hata kuzuia watoto kuhudhuria ibada ni sawa na kulemaza kanisa la siku za usoni.

Naye mhubiri maarufu Askofu J.B. Masinde wa kanisa la Deliverance Umoja jijini Nairobi alisema kanisa hilo halitafunguliwa kwa ibada na wataendelea kutoa mahubiri kupitia intaneti.

Askofu David Oginde wa CITAM pia ametangaza kuwa hawatafungua.

Wakuu wengi wa dini nchini ni wazee wa umri wa kuanzia miaka 60.

Katika kaunti ya Mombasa, waumini wengi Jumapili walidinda kuhudhuria ibada, hata baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kuwa makanisa yako huru kufunguliwa.

Wakizungumza na Taifa Leo, walisema sheria ambazo makanisa yaliagizwa kufuata ni ngumu.

Kwa maoni yake, Bw Simon Mwaniki ambaye ni mshirika wa kanisa la Jesus Celebration Centre (JCC), alisema kuwa alijihisi salama zaidi kufuatilia ibada akiwa nyumbani.

“Kwa maoni yangu, sheria hizo ni nyingi sana. Tumepewa jukumu la kujikinga wenyewe kutokana na virusi hivi na ni heri nisalie tu nyumbani ambapo bado nahubiriwa mtandaoni. Natuma sadaka kwa njia ya simu na cha muhimu zaidi, afya yangu nimeilinda,” akasema Bw Mwaniki.

Kwa upande wake, Collins Omondi ambaye ni mshirika wa kanisa la LifePoint, Mombasa alisema bado ana uwoga wa kutangamana na watu wengine.

Lakini katika Kaunti ya Kilifi, Mbunge wa Kilifi Kusini Ken Chonga, alianzisha shughuli ya kunyunyuzia dawa makanisani, huku akiitaka serikali iwakumbuke wahubiri ambao wanaendelea kuathiriwa na maambukizi ya corona.

Akizungumza katika eneo la Mtepeni alipowagawia chakula cha zaidi ya wahubiri 600 Bw Chonga alisema viongozi wa kidini wameathiriwa mno na kufungwa kwa makanisa, japo wengi wao wamekataa kujitokeza kuomba misaada.