Habari

Ni udhalimu kuongeza bei ya mafuta taa, Wakenya walia

May 7th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA PETER MBURU

WAKENYA wengi hawajafurahishwa na wazo la Tume ya Kudhibiti Kawi (ERC) nchini kutaka bei ya mafuta taa ipandishwe, na wanalichukulia kuwa hatua itakayowaadhibu Wakenya masikini, Taifa Leo imebaini.

Wakenya wanaitaka serikali kutochukua hatua hiyo kwani wanahisi itawaathiri vibaya watu wa mapato madogo, ambao ni sehemu kubwa ya taifa.

Wale waliohojiwa na Taifa Leo walisema kuwa endapo itachukuliwa, hatua hiyo itaishia kuwaumiza watu wasio na kazi, wenye mapato madogo, wazee katika jamii na masikini ambao kwa jumla wanaunda sehemu kubwa ya wakenya.

Walisema ni vikundi hivyo vinavyotumia mafuta taa kwa wingi kama mbinu ya kupata mwangaza nyumbani na pia kwa kupikia kwa stovu.

“Kupandisha bei ya mafuta taa kutaishia kuniathiri vibaya pamoja na maelfu ya Wakenya wenzangu ambao hatuna pesa kwani yanatusaidia katika shughuli za nyumbani. Ninayatumia kwa upishi kila siku,” akasema Joseph Mwaura, mfanyakazi wa vibarua mjini Nakuru.

Wengi wa waliohojiwa walisema mbeleni walitegemea makaa kwa upishi lakini wakahamia kutumia mafuta taa baada ya serikali kupiga marufuku ukataji miti kwa ajili ya kuchoma makaa.

Watu wengine walitilia shaka uwezo wa serikali kuleta bidhaa mbadala za kutosha kwa niaba ya mafuta taa na kwa bei itakayowiana na ya mafutaa kwa sasa.

“Watu wengi hupenda kutumia mafuta taa kwani bei yake ni rahisi na hivyo familia hutumia kama Sh30 pekee kwa siku au hata chini kupata mwangaza na kupika. Tunashangaa kama mbinu mbadala inazoahidi serikali zitakuwa rahisi hivyo ama zitakuja kuchukua pesa zaidi,” akasema Bi Angela Jeruto, mkazi wa Rongai.

Wakenya wengi, haswa maeneo ya mashambani ambapo umeme haujapenyeza na maeneo ambayo kupotea kwa nguvu za umeme ni hali ya kila siku bado wanatumia mafuta taa kwa wingi.

Wiki iliyopita, tume ya ERC ilirai serikali kupandisha bei ya mafuta taa kufikia ile ya dizeli, kama mbinu ya kuwakomesha Wakenya kununua bidhaa hiyo.

Kulingana na ERC, wazo hilo lilikuja baada ya kubaini kuwa matumizi ya mafuta taa nchini yamezidi kufikia kiwango cha lita milioni 33 kwa mwezi, ilhali inafaa kuwa chini ya lita milioni tano kwa kipindi hicho.

Mamlaka hiyo ilikosoa matumizi hayo ikisema zaidi ya asilimia 80 ya kiwango cha mafuta yanayotumiwa nchini kiliishia kwa magari, kutokana na hulka mbaya ya wanabiashara watundu kuchanganya bidhaa hiyo na mafuta ya dizeli na kuwauzia watumizi wa magari bila kujua.

“Zaidi ya lita milioni 27 zinaishia kutumiwa na magari jambo ambalo limeharibu magari mengi. Jambo hili aidha limeharibia Kenya soko la nje la mafuta ya dizeli na hivyo kuishia kupoteza ushuru wa Sh34bilioni,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa ERC Pavel Oimeke wiki iliyopita.

Kulingana na tume hiyo, kampuni kadhaa zitapewa kandarasi kusambaza bidhaa mbadala kwa bei iliyopunguzwa na serikali kama njia ya kupunguza ukali wa mabadiliko yanayotarajiwa.