• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:24 AM
Kipande cha ardhi kilichokuwa kimenyakuliwa Thika charejeshwa kwa serikali

Kipande cha ardhi kilichokuwa kimenyakuliwa Thika charejeshwa kwa serikali

WANYAKUZI wa ardhi ya umma wamepewa onyo kuwa hawatasazwa na serikali.

Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina amepongeza hatua zilizochukuliwa za kuchukua udhibiti wa kipande cha ardhi ya umma ambacho kilikuwa kimenyakuliwa mjni Thika.

Alisema ardhi ya karibu ekari moja eneo la Section 9 mjini Thika ilikuwa imenyakuliwa.

“Tayari nimesitisha unyakuzi huo katika afisi ya ardhi iliyoko Thika na eneo hilo litasalia kuwa la serikali. Hakuna mtu yeyote ataruhusiwa kunyakua kipande cha ardhi ya umma hapa Thika,” alisema Bw Wainaina.

Alisema tayari amewasiliana na Wizara ya Elimu na kupendekeza maabara ya wanafunzi kujengwa pahala hapo.

“Tunaelewa vyema kuwa hapa Thika bado hatuna maabara maalum ya kutosheleza matakwa ya wanafunzi ambao wamekuwa wengi kutokana na kuchipuka kwa vyuo na taasisi nyingi za elimu. Kwa hivyo, maabara ya kisasa kujengwa kutakuwa kwa manufaa,” alisema Bw Wainaina.

Alisema tayari ameanzisha vita maalum kupambana na wanyakuzi wa ardhi mjini Thika ambao wanaongezeka kila kuchao.

Ardhi hiyo iko katika eneo nzuri la mji wa Thika kwa sababu kipande chenyewe kiko katikati mwa mji huo.

Alisema tayari ilani ya kuonyesha kwamba kipande hicho ni cha serikali imewekwa pahala hapo ambapo hakuna yeyote kwa sasa anaruhusiwa kujenga ama kujifanyia jambo lolote katika eneo hilo.

Alisema kwa muda mrefu ameteta kuhusu unyakuzi wa ardhi lakini wengi wa watu walichukulia kama ni mzaha, lakini wakati huu ameamua kukabiliana nao “bila kujali huyu ni nani.”

“Nitaanza kuzuru sehemu tofauti katika eneobunge la Thika ili niweze kujua hasa ni kipande gani cha ardhi kimenyakuliwa ili tuweze kurudisha chini ya umma. Kwa muda mrefu watu wengi wamegeuza unyakuzi wa ardhi kama njia yao ya kujitafutia mali,” alisema Bw Wainaina.

Wakazi wa Thika tayari wamempongeza mbunge wao kwa kufanikisha hilo.

Bw James Njuguna ambaye ni mkazi wa Thika alisema ni jambo la kuridhisha kila mwananchi.

“Tumefurahi kusikia ya kwamba kipande cha ardhi ukubwa wa ekari moja kimerudishwa kwa umma, jambo ambalo lilikuwa ndoto hapo awali. Tungetaka wanyakuzi wa ardhi wachukuliwe hatua kali bila kuonewa huruma,” alisema Bw Njuguna.

You can share this post!

Oliech atetea bwanyenye wa Wazito

Harrison Mwendwa katika rada kali ya AFC Leopards

adminleo