• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 9:41 AM
Mafuriko yasukuma mzee kuishi juu ya mti

Mafuriko yasukuma mzee kuishi juu ya mti

Na VICTOR RABALLA

MIEZI minne baada ya janga la mafuriko kushuhudiwa nchini, mzee mwenye umri wa miaka 60 bado anaendelea kuishi juu ya mti katika kijiji cha Amboo, eneobunge la Nyando, Kaunti ya Kisumu.

Mzee Joseph Akong’o amejenga nyumba juu ya miti baada ya nyumba yake ya awali ya vyumba viwili kuharibika kiwango cha kutoweza kukarabatiwa tena.

Aidha anasema hana fedha za kujenga nyumba nyingine na hata akifanya hivyo, bado itakuja kusombwa na maji kama ile ya awali wakati wa mafuriko siku zijazo.

Mzee huyo ametumia mbao na mabati kujenga nyumba ya chumba kimoja juu ya miti kisha akaweka kitanda na baadhi ya samani.

Ili kufikia nyumba yake lazima usafiri kupitia boti kwa kilomita 2.5 kutoka majini hadi eneo kavu katika kituo cha kibiashara cha Amboo.

Usafiri huo hugharimu Sh20 kwa kila safari huku mzigo wa ziada ukiongeza kiwango cha ada inayotozwa.

“Nililazimika kurudi nyumbani baada ya mafuriko kuisha. Hata hivyo, nyumba hii inanisitiri kwa wakati huu kwa sababu ile ya awali iliharibika kiwango cha kutotengenezeka tena,” akasema.

Mafuriko hayo pia yalimtenga na wanawe ambao wametafuta hifadhi katika maeneo mengine kwa jamaa na marafiki ambao hawakuathirika.

“Baadhi ya watoto wangu wametafuta hifadhi katika shule ya upili ya Nduru huku wengine wakiishi na jamaa zangu maeneo ya Rabuor na Korowe,” akaeleza Taifa Leo.

Zaidi ya wakazi 6,000 wa eneo hilo pia bado wanaendelea kuishi kwenye kambi za muda.

Baadhi ya shule pia zimegeuzwa makazi ya watu ambao nyumba zao zilisombwa na mafuriko hayo baada ya maji ya kutoka Ziwa Victoria kuingia kwenye nyumba zao.

Kama njia ya kuwazuia watu wengi kukongamana eneo moja kwa muda mrefu katika kambi za muda, machifu, manaibu wao na wazee wa mitaa, hudhibiti idadi ya watu wanaoishi kwenye kambi hizo. Hii inatokana na hatari ya kupata virusi vya corona.

Katika maeneo mengine, mamia ya wanakijiji wamejenga nyumba zao juu ya vigingi vilivyotengenezwa ili kuzuia mafuriko kusambaa hadi makazi ya watu.

Karibu watu 32,000 walihama makwao kutokana na mafuriko katika eneobunge la Nyando baada ya mto Nyando kuvunja kingo zake kutokana na maji ya Ziwa Viktoria kujaa hadi pomoni.

Chifu wa Kawino Kusini, Bw Charles Abuto, alisema mafuriko bado yamezamisha nyumba kadhaa katika lokesheni ndogo za Ugwe, Nduru na Kadhiambo.

“Ni lokesheni ndogo ya Kwakungu pekee ambako baadhi ya wakazi wameanza kurejea polepole. Hata hivyo, hali bado ni mbaya na watu wanahitaji msaada wa vyakula, sodo, neti na blanketi,” akasema.

You can share this post!

Omar Lali aachiliwa

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Fadhila sufufu za Siku ya Ijumaa

adminleo