Habari Mseto

Madaktari 20 wa Cuba kupiga jeki vita dhidi ya Covid-19

July 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI ya Kenya imeomba msaada wa madaktari 20 kutoka Cuba kusaidia katika vita dhidi ya janga la Covid-19 hivi visa vya maambukizi vikipanda hadi 12,062 kufikia Ijumaa.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema madaktari hao wanatarajiwa kuwasili Ijumaa usiku na watakuwa wakitoa huduma zao katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTRH).

“Madaktari hawa ambao wana utaalamu katika nyanja mbalimbali za utabibu watafanya kazi kwa ushirikiano na madaktari wa Kenya kwa moyo wa ushirikiano kati ya Kenya na Cuba,” amesema alipowahutubia wanahabari katika Kaunti ya Murang’a.

Akaongeza: “Na madaktari hao watakuwa nchini kwa kipindi cha miezi sita. Baada ya hapo tutadurusu na kutathmini utendakazi wao ili kuona ikiwa bado tutahitaji huduma zao au la. Lengo la ushirikiano huu ni kuwezesha madaktari wetu kupata uzoefu wa kiwango sawa na watalaamu hawa.”

Mnamo 2018 Kenya madaktari 100 wa Cuba waliwasili nchini na kutumwa katika hospitali mbalimbali nchini kutoa huduma maalum. Kila hospitali ya rufaa ya Kaunti ilipata madaktari wawili chini ya mpango huo.

Bw Kagwe ameongeza kuwa chini ya mkataba huo, Kenya imekuwa ikiwatuma madaktari wake nchini Cuba kwa mafunzo zaidi katika nyanja mbalimbali za utabibu.

Kundi hilo la madaktari 20 wa Cuba ni wataalamu katika nyanja ya tiba ya saratani, ugonjwa wa moyo, magonjwa ya watoto na magonjwa mengine sugu.

“Huku idadi ya maambukizi ikiongezeka na wathiriwa wengi ni watu wenye magonjwa sugu, madaktari hawa watapiga jeki pakubwa juhudi za madaktari wetu za kukabiliana na matatizo hayo,” akaeleza Bw Kagwe.