Wakuzaji pamba kufaidi baada ya Rivatex kushirikiana na kaunti 20
WAKULIMA wa pamba katika maeneo ya Magharibi na Mashariki wanatarajia kunufaika na hatua ya kiwanda cha kutengeneza vitambaa cha Rivatex, mjini Eldoret, kuanza ushirikiano na kaunti 20 za maeneo hayo.
Kiwanda hicho kinalenga kuongeza kiwango cha ukuzaji pamba ili kupata mali ghafi ya kutosha kwa urahisi.Kiwanda huwa kinahitaji marobota 60,000 ya pamba kufanikisha uzalishaji wake, kinyume na sasa ambapo huwa kinapata marobota 10,000 pekee.
Kwa sasa, kinalazimika kuagiza asilimia 90 ya pamba ambayo huwa kinatumia ili kutosheleza mahitaji yake.Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Prof Thomas Kipkurgat, alisema kuwa ushirikiano huo utaongeza uzalishaji wa pamba nchini na kupunguza kiwango wanacholazimika kuagiza kutoka nje.
Alieleza wanaamini hatua hiyo itaongeza kiwango cha pamba wakulima wanazalisha nchini.
Alitaja kaunti za Baringo, Elgeyo Marakwet, Pokot Magharibi, Turkana, Busia, Vihiga, Teso, eneo la Nyanza na Kericho kama miongoni mwa kaunti ambazo wamebuni ushirikiano nazo.
Onyango K’onyango na Barnabas Bii