• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:47 PM
Waumini wagomea ibada wakiogopa corona

Waumini wagomea ibada wakiogopa corona

Na BENSON MATHEKA

WAUMINI wa makanisa mengi nchini walikosa kuhudhuria ibada makanisa yalipofunguliwa jana, huku idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona nchini kwa siku moja ikiendelea kuwa juu.

Wizara ya Afya ilitangaza kuwa watu 603 waliambukizwa na kufikisha idadi ya jumla hadi 13,353.

Idadi ya wagonjwa waliopona ilitimia 5,122 baada ya watu 682 kuthibitishwa kuwa wamepona. Hata hivyo, wengine tisa walifariki na kufikisha idadi ya jumla hadi 234.

Wizara ya afya ilisema kwenye taarifa kwamba watu 562 miongoni mwa waliopona walikuwa wakiuguzwa wakiwa nyumbani.

“Miongoni mwa waliopona, 562 walikuwa wakitibiwa nyumbani huku 129 wakiruhusiwa kuondoka kutoka hospitali mbalimbali,” ikasema taarifa.

Idadi ya maambukizi ya virusi vya corona imekuwa ikiongezeka kwa kasi tangu masharti ya kuzuia kusambaa kulegezwa Julai 6.

Mwigizaji wa vipindi vya runinga Charles Bukeko, maarufu kama Papa Shirandula ambaye ni miongoni mwa waliofariki kwa corona atazikwa leo. Kutokana na hali inavyoonekana kuzidi kuwa mbaya, Kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini Kadinali John Njue, jana aliwahimiza Wakristo kutumia kufunguliwa kwa makanisa kuomba Mungu amalize janga la corona.

Alikuwa akiongoza misa ya kwanza mbele ya waumini baada ya miezi mitatu katika Kanisa la Holy Family Basilica jijini Nairobi, ambayo pia ilihudhuriwa na watu wachache wasiozidi 100.

“Imekuwa zaidi ya miezi mitatu ambayo hatukuweza kukutana kwa ibada hata siku za Jumapili kama hii kwa sababu ambazo kila mtu anafahamu. Lakini tunashukuru Mungu, kwamba tumeweza kuwa na ibada ana kwa ana kama hii. Tunawakaribisha kwa misa hii, tunatambua na tunajua ni baraka,” aliwaambia waumini wasiozidi 100 waliohudhuria misa hiyo.

Aliwataka maaskofu na mapadre wa Kanisa Katoliki kuzingatia kanuni za wizara ya afya za kuzuia msambao wa virusi vya corona.

Mnamo Julai 6, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza maeneo ya ibada kufunguliwa kwa awamu kufuatia mwongozo uliotayarishwa na baraza la viongozi wa Kidini.

You can share this post!

Handisheki yageuza ‘Baba’ bubu

Serikali yajiandaa kwa hatua mpya kukabili corona

adminleo