• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Madiwani wapinga sheria kudhibiti maadili yao

Madiwani wapinga sheria kudhibiti maadili yao

Na FRANCIS MUREITHI

MADIWANI wamepinga sheria mpya ambayo inalenga kudhibiti maadili yao ndani na nje ya mabunge ya kaunti.

Baraza la Maspika wa Kaunti (CAF) limeenda katika Mahakama ya Kikatiba likiitaka kuingilia kati, baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutia saini mswada huo unaoruhusu madiwani wanaokiuka kanuni za maadili mema kung’olewa mamlakani.

Mswada huo, ambao uliwasilishwa na Seneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), ulipitishwa na Seneti Aprili 21 huku Bunge la Kitaifa likiupitisha Juni 30. Rais Kenyatta aliuidhinisha rasmi kuwa sheria Julai 9.

Kulingana na sheria hiyo mpya, madiwani watakuwa katika hatari kupoteza nyadhifa zao ikiwa watapatikana wakikosa adabu ndani au nje ya mabunge ya kaunti, kando na matumizi mabaya ya afisi, kupatikana na kosa lenye adhabu ya kifungo cha zaidi ya miezi sita kati ya sababu zingine.

Mwenyekiti wa baraza hilo, Bw Ndegwa Wahome, ambaye pia ni Spika wa Bunge la Kaunti ya Nyandarua, aliitaja sheria kuwa “yenye ubaguzi.”

Alisema kuwa ni kutokana na hatua hiyo ambapo wameamua kutafuta ufafanuzi wa mahakama kuhusu baadhi ya vipengele tata kwenye sheria.

“Tumeamua kwenda katika mahakama ya kikatiba ili kuiomba iingilie kati. Hofu yetu ni kuondolewa kwa hitaji la mahakama kutathmini uhalali wa malalamishi yanayowasilishwa ili kuwang’oa madiwani mamlakani,” akasema Bw Ndegwa.

Wakati huo huo, Bw Ndegwa aliikosoa sheria hiyo, akisema kuwa “inawaonea madiwani, kwani inaufanya mchakato wa kuwaondoa mamlakani kuwa rahisi kuliko Seneta, mbunge ama Mwakilishi wa Wanawake.”

Alisema hakuna sababu za kutosha kwa sehemu hiyo kutolewa, kwani imekuwepo kwenye Sheria Kuhusu Serikali za Kaunti.

Alisema kuwa ili diwani kutolewa uongozini, lazima mchakato huo uzingatie kanuni zote, mojawapo ikiwemo kutathminiwa kwa malalamishi yanayowasilishwa dhidi ya diwani na Mahakama Kuu.

“Ni kwa hilo tunataka kujua sababu ya kutolewa kwa kipengele hicho,” akasema.

Kando na hayo, alieleza kuwa maspika wengi katika kaunti hawakufahamishwa lolote kuhusu mswada huo, hivyo hawakushirikishwa kwenye maandalizi yake kama inavyotakikana na katiba.

“Sisi ndio wahusika wakuu kuhusu sheria hiyo kwani Maspika pia ni madiwani. Ushirikishi wa umma haukufanywa ifaavyo,” akasema Bw Ndegwa

Baraza lilisema kuwa linaamini litapata maamuzi yafaayo kutoka kwa mahakama kuzuia utekelezaji wake.

Sheria imezua wasiwasi miongoni mwa madiwani zaidi ya 3,400 kote nchini.

Katika Kaunti ya Nakuru, aliyekuwa Kiongozi wa Wengi, Bw Stanley Karanja, ambaye pia ni diwani wa wadi ya Naivasha, alisema madiwani wengi hawafahamu lolote kuihusu.

“Hii ni sheria yenye uzito na inayohitaji mawakili kuwafafanulia madiwani kuihusu. Tunapaswa kufahamu undani wake kwani inaonekana kutishia uhuru na haki ya wananchi kuwachagua viongozi wao,” akasema Bw Karanja.

Akaongeza: “Sheria hii imewafanya madiwani kuwa viongozi wasio usemi wowote. Huu ni usaliti wa wazi kutoka kwa Seneta Murkomen.”

Alimrai Spika Joel Kairu kupanga kikao ambako madiwani watatoa ufafanuzi kwa madiwani kuhusu sheria hiyo.

“Nitatoa nakala kwa madiwani kwani tuna mawakili katika Bunge. Watatupa ufafanuzi kamili,” akasema Bw Kairu.

You can share this post!

Serikali yajiandaa kwa hatua mpya kukabili corona

Familia yasisitiza kifo cha ‘Shirandula’ kingeepukika

adminleo