Mbinu ilizotumia Safaricom kuzoa faida ya Sh55 bilioni licha ya wimbi la #Resist
Na CHARLES WASONGA
KAMPUNI ya mawasiliano ya Safaricom ilipata faida ya Sh55.29 bilioni, baada ya kutozwa ushuru, katika mwaka wa kifedha uliokamilika Machi 31, 2018, kutoka Sh48.44 bilioni ilizoandikisha mwaka 2017.
Hii ni sawa na ongezeko la faida kwa kima cha asilimia 14.1.
Mapato yake ya jumla pia yaliimarika kutoka 212.9 bilioni mwaka 2017 hadi Sh233.7 bilioni mwaka huu, ongezeko linalowakilisha asilimia 9.8.
“Faida yetu iliendelea kuimarika 2017 licha ya changamoto za kiuchumi, ukame na kupanda kwa joto la kisiasa kufuatia kupindi kirefu cha uchaguzi,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji Bob Collymore Jumatano.
“Faida hii ya kima cha asilimia 14.1 inaashiria kuwa Safaricom ilimarisha usamamizi wa rasilimali zake huku ikidumisha huduma kwa wateja wake,” akaongeza afisa huyo Jumatano asubuhi alipohutubia wawekezaji wa kampuni hiyo kupitia teknolojia ya video ya mtandaoni.
Bw Collymore ambaye amekuwa katika likizo kupata nafasi ya kupokea matibabu alitangaza kuwa atarejea kazini hivi karibuni kwani afya yake imeimarika.
“Nasubiri idhini ya madaktari kabla ya kurejea nchini Kenya kuendelea na majukumu yangu,” akasema afisa huyo ambaye aliondoka nchini Oktoba mwaka 2017 kwenda Afrika Kusini kwa matibabu.
Safaricom pia iliungama kuwa hatua ya muungano wa upinzani (NASA) kuchochea wafuasi wake kususia huduma na bidhaa za kampuni hiyo Septemba mwaka 2017 iliathiri mapato yake “japo sio kwa kiwango kikubwa zaidi”.
“Siasa chafu za baada ya uchaguzi mkuu uliopita haswa zilitatiza soko letu la huduma za kupiga simu kati ya mwezi Septemba hadi Desemba 2017,” Bw Collymore akawaambia wawekezaji hao katika makao makuu ya kampuni hiyo, jumba la Safaricom, Westlands, Nairobi.
Sehemu kubwa ya faida ya Safaricom ilitokana na huduma za kupokea na kutuma pesa kupitia simu, maarufu M-PESA, ambayo iliiwezesha kupata jumla ya Sh62.9 bilioni kutoka Sh36.4 bilioni katika kipindi kama hicho 2017.
“Hii ina maana kuwa mapato huduma za M-PESA yaliimarika kwa kima cha asilimia 14.2 katika mwaka wa kifedha uliokamilika Machi 31 mwaka huu.
Huduma hii inachangia asilimia 28 ya mapato ya Safaricom,” Mkurugenzi wa Masuala ya Fedha Sateesh Kamash akasema alipowasilisha takwimu za matoke0 ya faida. Kufikia sasa wateja wa M-PESA wamefikia watu 2.1 milioni.
Bw Kamash alitangaza kuwa Safaricom itatumia kati ya Sh35 bilioni na Sh38 bilioni katika mwaka wa kifedha wa hadi Machi 31, 2019 kwa ajili ya kupanua mitambo yake ya kutoa huduma.
“Katika mwaka wa kifedha hadi 2019 tunatarajia kuimarisha mitandao yetu ya mawasiliano, huduma za data na mipango mingine ya kuiwezesha kampuni kuimarisha huduma zake na faida,” akasema.
Bw Kamath alisema bodi ya wakurugenzi wa Safaricom imeidhinisha mgao (dividends) wa Sh44.1 bilioni kwa wenyehisa wake.
Hela hizi zitalipwa kwa kiwango Sh1.10 kwa kila hisa.