Zimbabwe yarejesha kafyu
Na MASHIRIKA
ZIMBABWE imetangaza upya kafyu na masharti makali zaidi kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, baada ya visa vya maambukizi ya virusi kuongezeka.
Kuanzia jana, taifa hilo lilianza kutekeleza kafyu kutoka saa 12 jioni hadi saa 12 alfajiri, huku vikosi vya usalama vikiagizwa kumkabili yeyote atakayepatikana akikiuka kanuni hizo.
Watu ambao hawafanyi kazi watalazimika kukaa nyumbani, lakini wataruhusiwa kutoka nje wanaponunua vyakula na kutafuta matibabu.
Wafanyabiashara wataruhusiwa kuendesha shughuli zao kati ya saa mbili asubuhi na saa tisa mchana.Hata hivyo, wale wanaoendesha shughuli za dharura wataruhusiwa kuhudumu nje ya wakati huo.
“Hatuwezi kuruhusu hali kuendelea kudorora huku tukitazama. Lazima tuchukue hatua kali kudhibiti maambukizi,” akasema Rais Emmerson Mnangagwa, kwenye hotuba kwa taifa hilo.
Alisema kuwa yeyote atakayepatikana akikiuka kanuni hizo “atakabiliwa vikali.”Kufikia sasa, taifa limethibitisha visa 1, 820 vya virusi.
Wadadisi wa masuala ya afya wanasema kuwa ingawa idadi hiyo ni ya chini ikilinganishwa na mataifa mengine, imekuwa vigumu kwa madaktari nchini humo kudhibiti maambukizi kutokana na ukosefu wa vifaa vya kutosha.
Wiki iliyopita, idadi ya vifo iliongezeka kutoka 18 hadi 26, hali inayoonekana kuibua wasiwasi miongoni mwa maafisa mbalimbali serikalini.
Rais Mnangagwa alifunga shughuli za kiuchumi kwa siku 21 Machi 30. Kando na hayo, alipiga marufuku mikusanyiko ya watu wengi na kuwaagiza wafanyabiashara wote kufunga biashara zao.
Ni maduka ya kuuza vyakula pekee yaliyoruhusiwa kuendesha shughuli zake.Majuma machache yaliyofuata, makundi ya kutetea haki za binadamu yalilalamika kuwa wanajeshi na polisi walikuwa wakitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia kwa kisingizio cha kutekeleza kafyu.
Serikali iliondoa masharti hayo mwanzoni mwa Mei, hali inayotajwa kuchangia ongezeko la visa hivyo.Kwenye maagizo mapya, serikali haitawaruhusu watu zaidi ya 50 kukutana. Usafiri kati ya miji mbalimbali pia umepigwa marufuku.
Wakati huo huo, Rais Felix Tshisekedi wa DR Kongo ameondoa masharti yaliyokuwepo nchini humo kuhusu kudhibiti maambukizi ya virusi.
Hapo jana, aliagiza shule kufunguliwa upya, kurejelewa kwa shughuli za biashara na maeneo ya mipakani.Hata hivyo, ufunguzi huo utaendeshwa kwa awamu tatu.
Tangu Machi, taifa limethibitisha visa 8, 534 na vifo 196.Alisema kuwa kuanzia jana, maduka yote, benki, mikahawa na baa zitaruhusiwa kufunguliwa upya.
Shughuli za usafiri wa umma na mikutano ya watu wengi pia imeruhusiwa.
Alisema kuwa shule na vyuo vikuu zitarejelea shughuli za masomo kuanzia Agosti 3, huku viwanja vya ndege, bandari, mipaka na maeneo ya kuabudia yakirejelea shughuli zake Agosti 15.