MUTUA: Serikali haijali maslahi ya raia ndani na nje ya nchi
Na DOUGLAS MUTUA
MWANAHABARI Mkenya, Bw Yassin Juma, atapandishwa kizimbani nchini Ethiopia wiki ijayo kujibu mashtaka yanayoaminika kuwa ya kusingiziwa.
Kando na kwamba atakuwa kwenye mahakama ya nchi nyingine, Bw Juma atakabiliwa na changamoto tatu kuu: kutokuwa na wakili, kutoielewa lugha rasmi ya Ethiopia na kupuuzwa na Serikali ya Kenya.
Hiyo ni hali isiyotamanisha kwa mtu yeyote kujipata akikabiliwa nayo hata kama ametenda kosa gani.
Bw Juma, ambaye ni mwanahabari wa kujitegemea na mtaalamu anayewashauri watu kuhusu mawasiliano, alikamatwa mapema mwezi jana baada ya maandamano dhidi ya serikali ya Ethiopia ambapo yapata watu 240 waliuawa.
Alitiwa nguvuni alipopatikana nyumbani kwa mteja wake, Jawar Mohammed, ambaye ni mwanasiasa wa upinzani na mwanzilishi wa shirika la habari la Oromo Media Network (OMN).
Miongoni mwa matatizo niliyokwisha orodhesha hapo juu, la kukosa wakili ni la muda tu na labda kabla ya wakati huo mashirika ya kimataifa yatakuwa yamemtafutia uwakilishi tosha.
Lile la lugha pia huenda lisiwe hoja kwa maana iwapo atapata wakili mzuri Mwethiopia huenda akafanikiwa kupata mkalimani bora.
WIZARA YA MASHAURI YA KIGENI
Lakini tatizo la tatu ni kama ugonjwa wa saratani unaomla mgonjwa polepole japo kwa maumivu tele huku akijua fika kwamba pepo wa mauti anamnyelemea muda wote, hivyo karibuni anaelekea kaburini.
Mkenya yeyote aliyewahi kuwa na hitaji au kupata tatizo japo dogo namna gani atakwambia kuwa Bw Juma hana bahati! Wizara ya Mambo ya Nje na Serikali ya Kenya kwa jumla haijalikuhusu matatizo ambayo raia wake wanapata nje ya nchi!
Ingekuwa inajali, Bw Juma hangelala ndani siku mbili kwani juhudi za kidiplomasia, urafiki na ujirani mwema zingefanywa kuhakikisha yuko huru.
Ijapokuwa sasa Dkt Monica Juma si Waziri wa Mambo ya Nje tena, angetumia ushawishi wake kwa namna fulani kuisaidia Wizara hiyo kumtoa Bw Juma jela.
Nimetoa mfano wa Dkt Juma kwa sababu nakumbuka alitumika kama balozi wa Kenya nchini Ethiopia wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki, na hivyo lazima ushawishi wake nchini humo ulikita mizizi alipoteuliwa Waziri wa Mambo ya Nje na Rais Uhuru Kenyatta.
UFISADI KATIKA BALOZI
Rais Kenyatta mwenyewe anajulikana kuwa na uhusiano mzuri sana na watawala wa sasa wa Ethiopia na watangulizi wao, hivyo kumkomboa Bw Juma si kazi ngumu.
Lakini sijashangaa kwamba Serikali ya Kenya kwa jumla haijamfaa mwanahabari huyo wakati huu anapowahitaji zaidi.
Inavyoonekana ni kuwa kuna sera fiche ya kuwatelekeza Wakenya wanaojipata katika hali tatanishi nje ya nchi.Wakenya wanaoishi ughaibuni watakwambia hakuna kitu wanachochukia kama balozi za Kenya zilizo kwenye mataifa wanamoishi.
Ule mtindo wa maafisa wa serikali kujibeba kana kwamba kuwahudumia walipa ushuru ni kuwafanyia hisani ni maradhi yaliyoenea na kuvuka mipaka na bahari.Hata mtu anayetaka huduma za kawaida tu ubalozini huzungushwa akaishia kutoa ‘chai’.
Niliyashuhudia haya kwa macho yangu mwenyewe kwenye Ubalozi wa Kenya jijini Washington D.C, watu wakitoa hongo wapewe Huduma Namba!
Mtindo huu wa kuyakosea thamani na heshima maisha ya Wakenya, ndani na nje ya nchi, unapaswa kukomeshwa mara moja.
Hebu na tuanzie hapo pa Bw Juma, arejeshwe nchini bila masharti yoyote. Mwanahabari huyo ndiye mlezi wa ndugu zake mayatima na wao pamoja na familia yake changa wanamtegemea pakubwa.