• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Maskini kupigwa kiboko

Maskini kupigwa kiboko

Na CHARLES WASONGA

WATU wanaoishi katika kaunti maskini za Pwani, Kaskazini Mashariki na Ukambani wataendelea kuzama kwenye uchochole kutokana na pendekezo kuwa wapunguziwe mgao wa pesa za ugatuzi kutokana na idadi yao ndogo.

Hii ni baada ya kamati iliyokuwa imebuniwa na Spika wa Seneti, Ken Lusaka kutafuta mwafaka kuhusu suala hilo kushindwa kuelewana na ikabidi kikao cha kujadili ugawanaji huo kuahirishwa hadi wiki ijayo.

Iwapo hakutakuwa na mwafaka, kaunti hizo maskini hazitakuwa na lingine ila kukubali kupunguziwa pesa, ikizingatiwa kuwa ni maseneta 18 wanaopinga mfumo huo mpya wa ugawaji, na iwapo kura itapigwa watashindwa.

Maseneta kutoka kaunti hizo 18 ambazo kwa pamoja zitapoteza Sh17 bilioni, wamepinga mfumo huo, wakisema unahujumu manufaa ya ugatuzi.

Chini ya mfumo mpya uliopendekezwa na Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA), kaunti zenye idadi kubwa ya watu zitapata mgao wa juu ikilinganishwa na mwaka ulipita.

Kwa upande mwingine, kaunti za maeneo ya Kaskazini Mashariki, Pwani na Ukambani zenye idadi ndogo ya watu zitapata mgao mdogo.

Kaunti zitakazopoteza ni pamoja na Garissa, Wajir, Mandera, Marsabit, Isiolo, Mombasa, Kilifi, Lamu, Kwale, Tana River na Samburu.

Kwa mfano, Wajir itapoteza Sh2 bilioni, Mandera (Sh1.9 bilioni), Garissa (Sh1.6 bilioni), Tana River Sh1.5 bilioni na Mombasa Sh700 milioni.

Kaunti zingine ambazo zitapoteza ni Narok (Sh887 milioni), Isiolo (Sh879 milioni), Turkana (Sh450 milioni), Kitui (Sh219 milioni) na Makueni (Sh302 milioni).

Kwa upande mwingine, kaunti ambazo zimestawi zitaongezewa pesa ikiwemo Kiambu ambayo itaongezewa Sh1.3 bilioni, Nairobi (Sh1.2 bilioni), Uasin Gishu (Sh923 milioni) zaidi, Nandi (Sh788 milioni), Kajiado (Sh765 milioni), Nakuru (Sh744 milioni), Laikipia (Sh660 milioni) na Trans Nzoia (Sh655 milioni).

Kaunti zingine ambazo zitafaidi ni Kirinyaga (Sh538 milioni), Baringo (Sh537 milioni), Bomet (Sh456 milioni) na Pokot Magharibi (Sh444 milioni).

Baada ya maafikiano kukosekana kuhusu suala hilo, maseneta kutoka kaunti zinazopoteza walimlamu Spika Lusaka wakisema anapasa kuondolewa kwenye cheo.

Hii ni baada ya wanachama wa kamati hiyo – maseneta Irungu Kanga’ta (Murang’a), Mutula Kilonzo Junior (Makueni), Ledama Ole Kina (Narok) na Margaret Kamar (Uasin Gishu) kusema hawajapata mwafaka, Bw Lusaka aliahirisha kikao maalum cha jana.

“Nimeamua kuahirisha kikao cha kujadili na kuamua suala hilo baada ya wanachama wa kamati maalum niliyoteua kusaka muafaka kukosa kuelewana. Nimewapa muda zaidi ili walete ripoti yao Jumanne,” akasema.

Maseneta walikasirishwa na hatua hiyo huku baadhi yao wakimfokea Bw Lusaka kwa maneno makali.

Kelele za, “Aibu!” “Aibu!” zilitanda ukumbini pale Spika huyo alipoondoka baada ya kuahirisha kikao.

Muda mfupi baadaye, Seneta Kilonzo Junior alipendekeza Spika Lusaka ang’olewe mamlakani kwa kushindwa kufanikisha muafaka kuhusu suala hilo.

“Tunapaswa kumtimua Spika Lusaka kwa kuahirisha kikao cha Seneti kinyume cha sheria. Bure!” Bw Kilonzo Junior akaandika katika akaunti yake ya Twitter.

Mvutano kuhusu suala hilo umekwamishwa kupitishwa kwa Mswada wa Ugavi wa Fedha baina ya Kaunti ya 2020.

Kabla ya maseneta kupitisha mswada huo na kutiwa sahihi na Rais Uhuru Kenyatta, kaunti haziwezi kupokea fedha zozote kutoka Hazina ya Kitaifa.

Hii ina maana kuwa, kwa mfano, serikali za kaunti hazitaweza kuwalipa mishahara wafanyakazi wao mwishoni mwa mwezi huu ikizingatiwa kuwa magavana bado wanadai Sh30 bilioni za mwaka wa kifedha wa 2019/2020.

You can share this post!

Mahakama yawavua sita jukumu la usimamizi wa chuo na...

Kenya yamwomboleza Benjamin Mkapa

adminleo