• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Waiguru sasa adai Kibicho ndiye chanzo cha masaibu yake

Waiguru sasa adai Kibicho ndiye chanzo cha masaibu yake

Na WANDERI KAMAU

MZOZO wa kisiasa katika Kaunti ya Kirinyaga jana ulizidi kutokota, baada ya Gavana Anne Waiguru kudai kuwa Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Karanja Kibicho, anawafadhili madiwani kuvuruga serikali yake.

Kwenye barua ya wazi aliyomwandikia Jumatano, Bi Waiguru alimchemkia vikali Dkt Kibicho, akimtaja kuwa chanzo kikuu cha masaibu yote yanayoikumba serikali yake.

Bi Waiguru alidai kwamba Katibu amekuwa akiwapa maagizo madiwani kuhakikisha kuwa wanavuruga uongozi wake kwa kutumia kila njia.Alisema ni kutokana na maagizo ya Dkt Kibicho ambapo walijaribu kumng’oa mamlakani, na mzozo wa sasa, ambapo wamekataa kupitisha bajeti.

Kwenye barua hiyo, Bi Waiguru alidai kuwa na habari za kuhusu mkutano ambapo Dkt Kibicho alifanya na madiwani zaidi ya 20 kuhusu mpango wa “kusambaratisha kabisa utendakazi wa serikali yake.”

“Baada ya kufeli kwa njama za kuniondoa uongozini, sasa nimeshangaa kufahamu kuhusu mkutano uliofanya na zaidi ya madiwani 20 ambapo uliwarai kuendelea kuwa pamoja ili kusambaratisha serikali yangu,” akasema gavana huyo.

Alidai kuwa Katibu amewaahidi madiwani kutekeleza miradi ya maendeleo katika wadi zao, ambayo itafadhiliwa na serikali ya kitaifa.

Kulingana na Bi Waiguru, miradi hiyo ni uchimbaji wa visima vya maji katika kila wadi na ujenzi wa barabara utakaofadhiliwa na Mamlaka ya Ujenzi wa Barabara katika Maeneo ya Mashambani (KeRRA).

Gavana pia alimlaumu Dkt Kibicho kwa mpango wa “kuuteka” mchakato wa kampeni za Mpango wa Maridhiano (BBI) ili kumtenga kisiasa.

“Ninafahamu maagizo uliyowapa madiwani kuwa lengo lako kuu ni kutwaa uendeshaji wa mpango wa BBI mkiwa na Seneta Charles Kibiru (Kirinyaga),” akadai.

Hii ni mara ya kwanza kwa Bi Waiguru kumtaja hadharani Dkt Kibicho kuwa mhusika mkuu kwenye masaibu yanayomwandama.

Mwezi uliopita, madiwani 23 kati ya 33 walipiga kura na kupitisha hoja kumng’oa mamlakani Bi Waiguru, wakimlaumu kwa ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka.Hata hivyo, Bi Waiguru alinusurika baada ya Seneti kufutilia mbali hoja hiyo.

Lakini sarakasi hiyo ilionekana kuendelea, baada ya madiwani kwenda katika Mahakama Kuu, wakiitaka kufutilia mbali uamuzi wa Seneti.

Kupitia wakili Ndegwa Njiru, madiwani walisema kuwa Seneti haikuzingatia kwa kina ushahidi waliowasilisha kwake, licha ya kuthibitisha mashtaka yote.

“Uamuzi wa Seneti unaonekana kuwa na mapendeleo ya wazi. Tutafanya kila juhudi kuhakikisha tumewaokoa wakazi wa Kirinyaga dhidi ya kiongozi ambaye hajali maslahi yao,” akasema Bw Njiru.

Tayari, madiwani wamekataa kupitisha bajeti ya mwaka huu, wakimlaumu Bi Waiguru kwa “kutoyapa kipao mbele” maslahi ya wananchi.

Mapema mwezi huu, Bi Waiguru alitangaza kundi maalum la watu saba kumsaidia kusuluhisha mzozo huo lakini akaondoa majina hayo baadaye.

Wadadisi wanasema kuwa mzozo katika kaunti hiyo unaonekana kuchangiwa na siasa za kinyang’anyiro cha ugavana mwaka 2022.

Kando na Dkt Kibicho, baadhi ya watu wanaoonekana kumezea mate nafasi hiyo ni Mwakilishi wa Wanawake Wangui Ngirichi, kiongozi wa Narc-Kenya Martha Karua, balozi wa Kenya nchini Amerika, Bw Robinson Githae kati ya wengine.

You can share this post!

Barakoa na sanitaiza feki zafurika sokoni

Miezi mitatu wakiishi kichakani baada ya kukosa kodi

adminleo