Habari Mseto

Visa 5,000 vya dhuluma za kijinsia vyaripotiwa

July 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

Ongezeko la asilimia 7 ya visa vya dhuluma na vita vya kijinsia vimeandikishwa nchini kati ya mwezi Machi na Juni 2020, ikilinganishwa na kipindi sawa na hicho mwaka uliopita.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya Jumanne, katika kipindi hicho visa 5,000 vya dhuluma na ubakaji vimeripotiwa.

Miongoni mwa kaunti zilizotajwa kuathirika pakubwa ni pamoja na Nandi, Wajir, Lamu, Busia, na nyinginezo.

“Kaunti hizo zimeandikisha ongezeko la asilimia 30 ya dhuluma za kijinsia mwaka huu ikilinganishwa na kipindi sawa na hicho mwaka uliopita, 2019,” akasema Waziri Msaidizi katika Wizara ya Afya Dkt Mercy Mwangangi.

Kulingana na Waziri asilimia 70 ya visa hivyo, ni watoto walio chini ya umri wa miaka 18, asilimia 5 wakiwa jinsia ya kiume. “Waathiriwa wakuu ni watoto, na wamepokea matibabu katika vituo mbalimbali vya afya nchini,” Dkt Mwangangi akasema.

Ni ongezeko ambalo limetajwa kuchangiwa na athari za janga la Covid-19. Kisa cha kwanza cha corona kilithibitishwa nchini mnamo Machi 13, 2020.

Virusi vya corona vimechangia watu kupoteza ajira, Wizara ya Afya ikisema visa vingi vya dhuluma za kijinsia vinahusishwa na athari hizo, kwa kile imetaja kama watekelezaji kushindwa kukithi mahitaji ya kimsingi ya familia kama vile chakula.

Hata hivyo, serikali imeonya kuwa wahusika watachukuliwa hatua kali kisheria, ikisema janga la corona si kisingizio cha utekelezaji wa vita vya kijinsia na ubakaji.

“Changamoto hizo si kisingizio cha kutekeleza dhuluma za kijinsia,” akasema Waziri Mwangangi, akiibua suala la waathiriwa kuogopa kuenda hospitalini kutafuta matibabu kwa hofu ya kupitia unyanyapaa katika jamii.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali, Dianah Kamande ambaye ni mwasisi mwanzilishi wa shirika lisilo la kiserikali la Come Together Widows and Orphans Organization – CTWOO na anayefanya kazi kwa karibu na idara ya Masuala ya Kijinsia, alisema kati ya mwezi Machi hadi Juni, amepokea malalamishi 84 ya dhuluma za kijinsia.

Dianah ambaye pia mjane na mwathiriwa wa dhuluma hapo awali, alisema waathiriwa wakuu ni watoto na kina mama. “Kumekuwa na ongezeko la dhuluma za kijinsia tangu ugonjwa wa Covid-19 uingie nchini. Ninashauri wanawake, ikiwa ndoa yako imejawa na madhila, vita, ni muhimu utoke mara moja uokoe maisha yako,” akaelezea.

Huku waathiriwa wengi wakiogopa kuripoti madhila wanayopitia katika vituo vya polisi kwa hofu ya kupitia unyanyapaa katika jamii, Dianah alisema idara ya polisi ina afisi inayoangazia dhuluma za kijinsia na kwamba ni wajibu wa mwathiriwa kupata haki.

“Ukisharipoti ukabidhiwe nambari ya malalamishi (OB number), ulizia afisi inayoangazia dhuluma za kijinsia. Ina maafisa wenye utu na ambao watakuelekeza hatua utakazochukua kupata haki,” akashauri.

Pia alisisitiza haja ya kuwasiliana na idara ya kijinsia kupitia nambari za dharura, 1195 na ambazo hazitozwi malipo kuripoti dhuluma na vita vya kijinsia.

Dianah Kamande pia ni mmoja wa wakurugenzi wa Bodi ya kupambana na FGM nchini, na alisema si wengi wanaelewa hatua zinazopaswa kufuatwa kisheria, akihimiza haja ya hamasisho kufanywa.