• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 AM
2022: Hofu ya Jubilee kwa Raila yapanda

2022: Hofu ya Jubilee kwa Raila yapanda

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa Jubilee Jumatano walimsuta kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa kile walichotaja juhudi zake za kusababisha mgawanyiko kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto.

Viongozi hao walisema Bw Odinga, ambaye alidai Jumanne kwamba masuala yaliyomo kwenye mwafaka kati yake na Rais yanaweza tu kutekelezwa kupitia marekebisho ya Katiba, ana njama fiche ya kugawanya nyumba ya Jubilee “kutoka ndani”.

“Ni wazi kuwa Raila anamchukulia William Ruto kama mshindani wake na hii ndio maana anamchukia pamoja na wandani wake. Anajaribu kujionyesha kuwa rafiki wa Rais huku akionekana kumchukia Ruto. Anaendeleza siasa za mgawanyiko sio zile za kuunganisha nchi,” kiongozi wa wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen alisema, huku kauli yake ikionekana kuwakilisha msimamo wa kambi ya Ruto.

Seneta wa Nandi Samson Cherargei, ambaye ni mmoja wa wabunge wanaopinga marekebisho ya Katiba, vile alishikilia kuwa hamna haja kwa nguzo ya utawala kugatuliwa kupitia kubuniwa kwa nyadhifa zaidi kama afisi ya Waziri Mkuu mwenye mamlaka.

“Wanajua kuwa Ruto anaelekea kuwa Rais. Hii ndio maana sasa wanataka kufanyike kura ya maamuzi ili kuziua azma yake kwa kubuni wadhifa wa Waziri Mkuu ambao utatengewa watu fulani, na sio atakayechaguliwa moja kwa moja na Wakenya,” akasema Bw Cherargei.

Bw Ruto aliweka gizani kuhusiana na mazungumzo kati ya Rais na Raila hadi mwafaka huo ulipotangazwa mnamo Machi 9.

Na ingawa Naibu huyo wa Rais ameunga mkono mwafaka huo, akiutaja kama ambao utaunganisha nchini, amepinga kabisa wazo la Bw Odinga la kwamba ili mwafaka huo uzae matunda sharti katiba ifanyiwe mageuzi.

Mnamo Jumanne Bw Odinga aliwataka wafuasi wa chama chake cha ODM kuunga mkono mwafaka huo. Lakini akashikilia kuwa ili ufanikishwe sharti katiba ifanyiwe marekebisho kubuni wadhifa wa Waziri Mkuu sawa na ilivyopendekezwa kwenye rasimu ya Katiba ya Bomas iliyoandaliwa mnamo 2005.

Vile vile, Bw Odinga amependekeza kuanzishwe kwa utawala wa maeneo huku serikali za kaunti na ile ya kitaifa zikiendelea kudumishwa.

Kile ambacho kambi ya Ruto inahofia ni kwamba mabadiliko yoyote wa kimuunda na mamlaka ya Rais yataathiri nafasi ya Naibu Rais kuweza kufurahia mamlaka sawa na bosi wake, Rais Kenyatta, endapo atashinda urais.

Duru zinasema kuwa wafuasi wa Ruto pia wameingiwa na wasiwasi kwamba kura ya maamuzi huweza kubuni vuguvugu za kisiasa ambazo huenda zikavuruga nafasi ya Ruto kuingia Ikulu.

Lakini Bw Odinga anapinga wazo hilo: “Endapo mabadiliko ambayo yako katika mwafaka (MoU) hayatatekelezwa, uchaguzi mkuu wa 2022 utakumbwa na vurugu. Utajaa mkanganyiko, ghasia ya baadhi ya watu watavunjika moyo. Tunajaribu kuzuia hali kama hiyo,” Bw Odinga akasema alipohutubia wanachama wa Baraza Kuu (ODM) katika hoteli moja eneo la Elementaita, Gilgil.

Akaongeza: “Salamu kati yangu na Rais haikuhusu uchaguzi wa 2022. Lengo kuu lilikuwa kuunganisha nchini ili kuzua machafuko yalyoshuhudiwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana. Kwa hivyo, jambo hili halifai kufasiriwa kumaanisha kuwa nia ilikuwa ni kutoa nafasi kwa watu fulani kung’angania nyadhifa za uongozi.”

Kauli za Bw Cherargei zinafanana na zile za Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa ambaye majuma mawili yaliyopita alidai kuwa mwafaka huo “umekufa” iwapo ulinua kufanikisha marekebisho ya katiba kupitia kura ya maamuzi.

 

Salamu imeyeyuka

“Salamu imesambaratika. Haipo tena. Hatutaki kura ya maamuzi; ilhali wao wanataka kura ya maamuzi. Kwa hivyo, hatuwezi kulala katika kitanda kimoja. Vile vile, hatuwezi kukubali kubuniwa kwa ngazi nyingine ya utawala- itakuwa ghali mno,” Bw Duale akasema bungeni akirejelea pendekezo la Bw Odinga kwamba sharti katiba ifanyiwe mabadiliko.

Katika mwafaka huo, Rais na Odinga walikubaliana kushughulikia masuala kama; uhasama wa kikabila, ukosefu wa maadili ya kitaifa, ujumuishaji wa wote katika utawala, uimarishaji wa ugatuzi, kukomeshwa kwa chaguzi zenye kuleta migawanyiko, kuhakikisha usalama wa Wakenya wote, kumaliza ufisadi na kuhakikisha uwepo na ustawi shirikishi.

Kulingana na Bw Odinga baadhi ya masuala haya “sharti yashughulikiwe kupitia mageuzi katika sheria na katiba”.

Masuala hayo ni kama vile ujumuishaji ambapo kila eneo, kabila, dini au tabaka la Wakenya watahisi kuwakilishwa katika uongozi wa nchini.

Lakini Murkomen anasema: “Kura ya maamuzi ni mbaya kuliko uchaguzi na alivyosema Raila sharti ifanyike ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. Anaonekana kama mtu anayepigia debe siasa za udikteta,” akasema Bw Murkomen.

Naibu Kiranja wa Wengi katika Seneti Irungu Kang’ata anasema: “Nilisema Raila ana malengo fiche…. Bado simwamini”.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju alitoa kauli isiyo kali.

“Ni vizuri kwamba Wakenya wanaongea. Hii ni hatua muhimu na hatupasi kunyamazisha yeyote mwenye maoni tofauti na yetu. Tuweke masuala hayo yote kwenye meza. Na kama hakuna meza, kunaweza kutengeneza meza,” Bw Tuju akasema.

Kwa upande wake Naibu Kiongozi wa ODM Wycliffe Oparanya alisema ingawa chama hicho hakilengi uchaguzi wa 2022 kwa sasa, sio makosa kwa Bw Odinga kuwania urais wakati huo.

“Mbona watu wameingiwa na hofu kwamba Raila Odinga atawania urais. Yeye ni Mkenya na ana haki ya kufanya hivyo… hahitaji ruhusu kutoka kwa mtu. Kile anachohitaji ni kuidhinishwa na chama chetu,” Oparanya ambaye ni Gavana wa Kakamega, alisema alipohojiwa katika runinga.

You can share this post!

Mwanahabari abubujikwa na machozi baada ya kuponea...

#NaniKamaMama: Shiriki shindano la kumshindia mama Sh8,000

adminleo