HabariSiasa

Sonko azomewa kwa kudai kuwa alileweshwa Ikulu

July 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

GAVANA wa Nairobi Mike Sonko ametakiwa akomeshe sarakasi za kutisha kutamatisha mkataba wa kuhamisha baadhi ya majukumu ya serikali yake kwa serikali ya kitaifa bila kufuatia utaratibu uliowekwa.

Mawakili wanasema kwamba kulingana na mkataba huo, ni vigumu kwa Bw Sonko kujiondoa katika mkataba huo.Mnamo Ijumaa, Bw Sonko alikariri kwamba atatamatisha mkataba hu akilaumu Mkurugenzi wa Huduma za Jiji la Nairobi (NMS), Meja Jenerali Mohamed Badi, kwa kuupuuza.

Bw Sonko ambaye amekuwa akizozana na Bw Badi alidai alileweshwa na maafisa wa Ikulu ya Nairobi kabla ya kutia sahihi mkataba huo.Madai hayo yalijiri baada ya Bw Badi kumzuia kutumia nyumba rasmi ya gavana wa Nairobi iliyorejeshewa serikali yake na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

Kulingana na Bw Badi, nyumba hiyo iliyoko mtaani Lavington ni mali ya NMS kwa sababu Sonko alihamisha masuala ya ardhi kwa serikali kuu.

Wakenya walionekana kumuunga mkono Bw Badi wakisema Sonko anaendeleza sarakasi baada ya kubaini alikabidhi serikali kuu nguvu zake kama gavana.

“Mike Sonko anaharibu wakati wake kusema atajiondoa katika mkataba huo. Kipindi chake cha kuhudumu kama gavana mwenye nguvu kiliisha alipotia sahihi mkataba huo,” alisema Bw Luis Kwany, wakili jijini Nairobi.Alisema kwamba Sonko alijimaliza kwa sababu mkataba huo unasema ikiwa kuna mzozo kati ya pande zote mbili, utasuluhishwa kupitia kamati maalum.

Kamati hiyo ikishindwa kupatanisha pande zote, mzozo huo unafaa kuwasilishwa kwa kikao cha ushirikiano wa serikali za kaunti na serikali ya kitaifa ambayo inasimamiwa na Rais Kenyatta mwenyewe.

“Sioni Sonko akifaulu. Anafaa kusubiri hadi 2022 mkataba huo utakapokamilika na aombe Rais Kenyatta astaafu,” alisema.

Mtaalamu wa masuala ya usimamizi, Bw Abiud Makori, anasema kwamba madai ya Bw Sonko kwamba alileweshwa akiwa Ikulu hayatamsaidia.“Sonko anafaa kufahamu kwamba sarakasi zake hazitamsaidia.

Alipokuwa akilewa Ikulu, Rais Kenyatta na Raila Odinga walikomboa Nairobi kwa kuiweka chini ya Badi ambaye amefanya mengi katika muda mfupi,” alisema akiashiria kwamba kiongozi wa chama cha ODM huenda alihusika katika mipango ya kutwaa majukumu kutoka kwa Sonko.

Hata hivyo, wafuasi wa Sonko wanasema kuwa ana haki ya kujiondoa katika mkataba huo iwapo serikali ya kitaifa haijautekeleza kikamilifu waliyoafikiana.

Kulingana na Sonko, alitia sahihi mkataba huo kwa sababu ya heshima yake kwa Rais Kenyatta na kwamba wote wawili walikuwa na nia njema kwa wakazi wa Nairobi.

Hata hivyo anasema kwamba Bw Badi ambaye ni mwanajeshi amekuwa akitumia mabavu badala ya kuheshimu mkataba huo.

“Huyu mwanajeshi akiendelea hivi na kukataa kuheshimu sheria, heri wanitimue walivyomtimua Waititu (aliyekuwa gavana wa Kiambu) lakini sitakubali vitisho zaidi. Anasahau kwamba hii ni kandarasi na inaweza kutamatishwa wakati wowote,” alisema Bw Sonko.

Hii ni mara ya pili kwa Bw Sonko kutisha kutamatisha mkataba huo baada ya kugundua kuwa alikabidhi serikali kuu mamlaka yake alipoikabidhi majukumu muhimu ikiwa ni pamoja na ukusanyaji ushuru, afya, ardhi na ujenzi.