• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wakulima wa pamba Yatta wapokea Sh2 milioni

Wakulima wa pamba Yatta wapokea Sh2 milioni

Na LAWRENCE ONGARO

WAKULIMA wa pamba eneo la Yatta, Kaunti ya Machakos, wanajivunia kupata mavuno ya juu msimu huu.

Wakulima hao wana jambo la kujivunia baada ya kampuni ya Thika Cloth Mills Ltd kununua pamba yote waliovuna.

Mwaka 2019 wakulima hao walianza kufanya kilimo cha pamba kinyume na hapo awali ambapo eneo hilo lilikuwa kavu bila kupandwa chochote.

Ni kampuni ya Thika Cloth Mills iliyowahimiza wakuze mipamba kupata pamba. Ilifanya hivyo kwa kuwapa mbegu, mbolea, na dawa za kunyunyuzia ili kuboresha ukulima wao.

Katika muda wa wiki moja iliyopita, kampuni hiyo ilipiga kambi katika maeneo ya Yatta, na Ndalani ambapo ilinunua pamba kutoka kwa wakulima zaidi ya 100 ambapo iliwalipa takribani Sh2 milioni kwa mavuno ya pamba.

Wakulima wengi wanadai kuwa wakati kulikuwa na zuio la kusafiri na kafyu, watu wengi walipata masaibu mengi kwa kukosa fedha.

“Wakati huo tulikuwa tayari tumevuna pamba lakini wanunuzi wakashindwa kufika sehemu hizi,” akasema mkulima wa eneo hilo Bw Nzuki Ndonye.

Anasema zao hilo lilikuwa huko miaka za 70 lakini vyama vya ushirika vilisambaratika.

“Baadaye wakazi wa eneo hili waliamua kupanda mahindi na maharage, lakini hayakufanya vyema kwa sababu ya ukosefu wa mvua ya kutosha,” akaeleza Bw Ndonye.

Naye Bw David Kioko ambaye ni mkazi wa Yatta alipongeza serikali kwa kukubalia wakazi hao kupanda pamba ambayo imeweza kunawiri.

Bw David Kitiku ambaye ni mkulima mashuhuri eneo hilo anasema alipokea Sh50,000 kutokana na zao hilo huku akijivunia kuwa na ekari mbili alizopanda mipamba.

“Hata ninatamani kupanda mipamba mingine katika shamba la ukubwa wa ekari nne kwa sababu mahindi na maharage tumepanda kwa muda mrefu,” alisema Bw Kitiku.

Wakulima hao wameiomba serikali kuwatuma maafisa wa kilimo ambao watashauriana na wakulima kuhusu upanzi wa zao hilo.

Meneja mkuu wa kampuni ya Thika Cloth Mills Ltd, Bw Dickson Kariuki alisema kampuni hiyo ina uwezo wa kupokea hadi tani 10,000 kutoka kwa wakulima hao katika kaunti nzima ya Machakos.

Alisema tayari wameingia katika mkataba na wakulima wa Kaunti ya Lamu, Meru, Homa Bay, Kisumu na Siaya ili wanunue pamba kutoka maeneo hayo.

“Tumewahimza wachukue jukumu la kuzingatia kupanda mipamba kupata pamba kwa wingi kwa sababu kiwanda chetu kinashona nguo kiwango kikubwa,” alisema Bw Kariuki.

Kampuni hiyo hushona sare za maafisa wa usalama, vikoi, vitenge, na majora ya nguo.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bi Tejal Dodhia alisema wakati huu wa janga la corona kulikuwa kugumu kwao lakini serikali iliwapa zabuni ya kuunda sare za maafisa wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori ( KWS) na barakoa.

“Tunashukuru serikali kwa kujali maslahi ya wafanyakazi kwa sababu sasa kuna jambo la sisi na wao kujivunia,” alisema Bi Dodhia.

Alisema wafanyakazi walikuwa wamepewa likizo kwa sababu ya homa ya corona lakini wamerejea kazini na hiyo ni afueni kwao.

You can share this post!

Babu Owino sasa ni mfano tosha wa ‘mui huwa...

Walevi kuwindwa hata katika nyumba zao

adminleo