Habari Mseto

Walevi kuwindwa hata katika nyumba zao

July 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

WAZAZI wenye mwenendo wa kubugia pombe mbele ya watoto wao wakati huu wa janga la Covid-19, sasa watachukuliwa hatua za kisheria, Mamlaka ya Kupambana na Vileo na Mihadarati (NACADA) imeonya.

Mamlaka hiyo imewataka Wakenya kuripoti visa hivyo kwa afisi zake ili wahusika waadhibiwe ipasavyo.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Mwenyekiti wa NACADA, Prof Mabel Imbuga alisema wamechukizwa na ongezeko la visa vya watu kunywa pombe majumbani wakati huu ambapo serikali imefunga baa ili kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona.

“Tabia hii inawaweka watoto na vijana katika hatari ya kuingilia uraibu wa pombe. Mwenendo huu unavuruga mazingira bora ya wanafunzi kusoma nyumbani na watu kama hawa wanafaa kuadhibiwa,” akakasema.

Profesa Imbuga alitoa wito kwa umma kuripoti visa kama hivyo kwa NACADA kupitia nambari ya simu isiyolipiwa ya 1192.

“Pia watu watoe ripoti kama hizo kwa afisi zozote za maafisa wa utawala wa mkoa,” mwenyekiti huyo akaongeza.

NACADA inawataka wazazi “kuhakikisha kuwa pombe hairuhusiwi katika mazingira ya nyumbani ili waweze kupalilia uhusiano wa karibu na watoto wao.

Profesa Imbuga alitaja tafiti ambazo zimefanywa na mamlaka hiyo, ambazo zimefichua kuwa mienendo ya wazazi kunywa pombe mbele ya watoto wao ndiyo chimbuko la visa vya matumizi ya pombe na mihadarati miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi na za upili.

“Hii inaonyesha kuwa mazingira ya nyumbani yamegeuka kuwa hatari kwani wengi wa wanafunzi waliohojiwa katika tafiti hizo walikiri kuiga uraibu wa kutumia pombe na dawa za kulevya kutokana kwa wazazi na wakubwa wao nyumbani,” akaeleza.

Wizara ya Afya imetangaza kuwa imeandaa kanuni zinazolenga kupiga marufuku uuzaji wa pombe katika mikahawa, maduka ya jumla ya maeneo mengine ya umma.

Kanuni hii itaaathiri pakubwa biashara ya pombe endapo itapitishwa na kuanzia kutekelezwa. Hii ndio maana hatua hiyo imepingwa na wadau kama vile chama cha wamiliki wa baa nchini.