• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:47 AM
Musalia, Wetang’ula wataka hakikisho kuhusu sukari

Musalia, Wetang’ula wataka hakikisho kuhusu sukari

Na DENNIS LUBANGA

KIONGOZI wa Chama cha Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya, Moses Wetang’ula, wameitaka serikali kutoa ushahidi kuhusiana na hatua yake ya kuokoa viwanda vya sukari.

Hii ni kufuatia tangazo kuwa Serikali itafutilia mbali deni lenye thamani ya Sh62.5 bilioni katika viwanda hivyo.

Hatua hiyo itasaidia kuboresha hali katika ukanda huo wa sukari ikiwemo ethanoli, kawi na bidhaa nyinginezo za kuongezwa thamani.

Hata hivyo, Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula sasa wanaitaka serikali kutoa ushahidi kuhusu mpango wa kufutilia mbali madeni hayo.

“Ikiwa wamemaanisha kuhusu hatua ya kufutilia mbali madeni basi swali ni je, nyenzo muhimu za hatua hiyo ziko wapi?” Mabw Mudavadi na Wetang’ula walihoji kupitia taarifa ya pamoja.

Wanasiasa hao wanataka utambulisho dhahiri na uorodheshaji wa madeni yote ya kampuni zote za sukari kabla mchakato wa kufutilia mbali madeni hayo kubainishwa dhahiri.

Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula wametaka kujua kwa nini warasimu wangali katika kampuni ya sukari ya Mumias iwapo serikali inania ya kweli ya kufutilia mbali madeni hayo.

“Mrasimu alikuja kwa sababu kiwanda cha sukari kina madeni mengi na hakiwezi kutekeleza majukumu yake. Ni jambo linalokinzana kwa mtu kusema madeni yamefutiliwa mbali ilhali mrasimu angali Mumias,”alisema Bw Mudavadi.

Bw Wetang’ula aliwashtumu baadhi ya viongozi kutoka eneo hilo wanaozunguka na ajenda za maendeleo ambazo haziwezi kutekelezwa.

“Fikra zao ambazo hazitafaulu ni kwamba wataweza kuwahadaa watu na mipango ya kimaendeleo isiyo kuwepo. Kwa bahati njema watu wetu wako chonjo na hawawezi kulaghaiwa,” alisema Bw Mudavadi.

Mageuzi

Maoni ya viongozi hao wawili yameungwa mkono na viongozi wa mashinani katika eneo la Bonde la Ufa wakiongozwa na Bw Nick Mbaka, Bw Micah Kigen, Bw Fred Shabati, na Bw Yussuf Keittany.

“Tunaunga mkono kabisa maoni ya Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula kwa sababu tunaamini ni ya dhati kuhusu uchumi na nchi kwa jumla,” alisema Bw Mbaka.

Akitangaza misururu ya mageuzi katika kiwanda cha sukari Kilimo House, Nairobi, wiki mbili zilizopita, Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya, alisema serikali pia imeafikia kubinafsisha viwanda vitano vinavyomilikiwa na serikali ambavyo vinakumbwa na matatizo, kupitia mkataba wa muda mrefu.

Viwanda hivyo vinavyojumuisha Chemelil, Nzoia, Nyanza Kusini, Miwani na Muhoroni, vinaendeshwa na mrasimu.

Bw Munya alisema wazo la kukodisha linatokana na kuwa serikali itawaalika wawekezaji walio na tajriba katika kiwanda cha sukari kimataifa.

You can share this post!

Nusura Klopp avunje rekodi ya Guardiola

Familia yasema Mkapa alifariki kutokana na mshtuko wa moyo

adminleo