Habari Mseto

Uhuru aonya kliniki za mpango wa uzazi

July 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MWANGI MUIRURI

RAIS Uhuru Kenyatta ameamrisha makamishna wa kaunti watie nguvuni wahudumu wa afya katika hospitali za wamiliki binafsi na pia za serikali wanaowapa wasichana huduma za upangaji uzazi.

Kamishna wa Kaunti ya Murang’a, Bw Mohammed Barre, alithibitisha kuwa alipokea amri hiyo ya rais na tayari amewafahamisha machifu na manaibu wake kuwa macho nyanjani.

“Ni wazi haifai kumpa mtoto huduma za upangaji uzazi. Kuna wazazi ambao ‘wanakinga’ familia zao dhidi ya aibu ya msichana wao kupata mimba ya mapema. Hiyo ni leseni ya kumpa nafasi mtoto kujiingiza katika ngono kiholela,” akasema.

Mshirikishi wa Usalama katika ukanda wa Rift Valley, Bw George Natembeya pia alithibitisha kuwa eneo lake limepokezwa amri hiyo na tayari amezindua mikakati ya kuitekeleza.

“Kuna changamoto kwani hata ya baadhi ya wahudumu wa afya hutoa huduma za tohara ya wanawake wakiwemo wasichana wachanga. Hiyo ni amri ambayo nitaitekeleza kwa msingi kuwa imetolewa na Rais, na pia kwa msingi kuwa naamini ni haki kuwalinda wasichana wetu wachanga,” akasema.

Imebainika Rais alitoa agizo hilo kwa kuwa huduma hizo za upangaji uzazi zinachangia pakubwa ongezeko la visa vya wasichana wachanga kujiingiza katika ngono kiholela, na wengi wao huishia kushika mimba wakiwa wangali watoto.

Naibu Waziri wa Elimu, Bw Zack Kinuthia alisema kuwa ilani hiyo inalenga kuzuia wanaume kuwahadaa wasichana wadogo na kuwadhulumu kingono.

“Rais amefikia uamuzi huo baada ya kusaka ushauri wa kina kuhusu mimba za mapema kwa wasichana wachanga nchini ambazo zimegeuka kuwa janga. Aidha, visa vya wasichana wa umri mdogo kuolewa na wengine kuonekana katika hali za kuavya mimba vimechangia kero kwa rais na kuishia amri hiyo,” akasema.

Akiongea katika Kaunti ya Murang’a, Bw Kinuthia alisema kuwa rais alishauriwa sheria hairuhusu mtu binafsi, kikundi wala taasisi kutoa huduma za upangaji uzazi kwa watoto.