Mpinzani wa Magufuli ataka wafuasi wake wasitishwe
Na LOUIS KOLUMBIA
DAR ES SALAAM, Tanzania
NAIBU Mwenyekiti wa chama cha Chadema nchini Tanzania, Tundu Lissu, amewataka wafuasi wa chama hicho wasiogope vitisho vya “kudhulumiwa” akisema kutendewa hivyo kutawafanya tu kuwa na nguvu zaidi.
“Dhahabu ni sharti ipitie motoni ili ing’ae,” aliwaeleza wafuasi wa Chadema katika makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam.
Lissu – aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki – alizungumza na wafuasi wa chama hicho na wanahabari punde baada ya kuwasili nchini humo kutoka Ubelgiji ambapo amekuwa akipokea matibabu kufuatia majeraha ya risasi aliyoyapata mjini Dodoma mnamo Septemba 7, 2017.
Siku ya tukio hilo, watu wasiojulikana waliojihami kwa bunduki walimiminia risasi gari la Lissu nje ya nyumba yake Dodoma.
Lissu, aliyekuwa amechukua fomu za uteuzi kwa lengo la kupata uidhinishaji wa chama ili kumkabili Rais John Magufuli katika azma yake ya kuchaguliwa tena katika Uchaguzi Mkuu mnamo Oktoba 28, aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), mwendo wa saa nane kasoro dakika ishirini.
Wafuasi wa Chadema na wanaomuunga mkono Lissu, walifurika katika uwanja wa ndege na kumsindikiza hadi katika makao makuu ya chama cha upinzani mjini Kinondoni.
Waliwasili katika makao makuu hayo saa kumi na mbili jioni ambapo alianza kuwasilisha ujumbe wake.
Alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake kumshukuru Mungu, uongozi wa chama chake, Wakenya, Wabelgiji na jumuiya kimataifa kwa jumla, huku wakati uo huo akifafanua jinsi mwili wake ulivyokuwa baada ya tukio hilo.
“Mungu wetu ni mwema! Mungu wetu ni mwema,” aliimba.
“Katika hali ya kawaida, sikutarajiwa kuishi. Sikutarajiwa kuwa nanyi hapa. Lakini kwa kuwa Mungu wetu amejawa na neema, sasa niko hapa pamoja nanyi. Sasa ninaweza kutembea lakini sikufaa kuwa hai,” alisema.
Alisema mwili wake ulikuwa umejaa makovu na vichuma.
“Nikivua nguo hapa, nyinyi nyote mtatoroka. Mwili huu, isipokuwa kichwa na uso ni ramani ya makovu kutokana na risasi na makasi ya madaktari. Mwili huu una vipuli vingi vya vyuma siwezi kuelezea,” alisema.
Alisema risasi moja ilikuwa ingali mwilini lakini madaktari walisema ilikuwa salama zaidi ikisalia ndani kuliko kujaribu kuitoa.
“Mwili huu una matatizo mengi mno. Mungu wetu ni mwema na niko hapa nikitembea. Mungu wetu ni mwenye haki. Siwezi kupiga magoti na mkono mmoja hauwezi kunyooshwa lakini Mungu wetu ni mwema,” alisema.