Ruto awataka maseneta waandae mfumo 'rafiki' wa ugavi wa fedha
Na CHARLES WASONGA
NAIBU Rais William Ruto amewataka maseneta kuandaa mfumo wa ugavi wa fedha kwa kaunti utakaohakikisha kuwa kaunti zote zinafaidi.
Amesema mfumo huo haufai kutoa dhana kwamba kuna baadhi ya kaunti ambazo zinahisi kutengwa au kupokonywa fedha.
“Serikali ya Kenya ni serikali ya wananchi wote walioko pembe zote za nchi. Ni serikali ya walio wengi na walio wachache au wale ambao walitengwa miaka ya nyuma. Ndiposa wanasihi maseneta wetu wanapojadiliana kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha walenge kuunganisha taifa letu,” Dkt Ruto amesema Ijumaa.
Amesema hayo katika eneobunge la Aldai, Kaunti ya Nandi, alipohudhuria hafla ya mazishi ya Mama Hellen Serem, mamake mbunge wa eneo hilo, Cornelly Serem,
Kulingana na Dkt Ruto, maseneta wana uwezo wa kuandaa mfumo wa ugavi wa fedha utakaohakikisha kuwa hamna kaunti yoyote miongoni mwa 47 itakayohisi kupoteza ili nyingine ifaidi.
Naibu Rais ameungama kuwa ni wajibu wa kikatiba wa seneti kuamua mfumo bora wa kugawanya rasilimali miongoni mwa kaunti lakini akasisitiza kuwa sharti itekeleze wajibu huo kwa njia ya haki.
“Mfumo ambao wote wanaibuka washindi unaweza kupatikana. Lakini ule ambao utawaacha wengine wakihisi kupoteza ili wengine wafaidi, utaishia kuligawanya taifa,” Dkt Ruto akaongeza.
Maseneta wanatarajiwa kurejelea mjadala kuhusu suala hilo mnamo Jumanne, Agosti 4, 2020, ambapo watashughulikia hoja ambayo iliwasilishwa na Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja.
Hoja hiyo inapendekeza mfumo ambapo hamna kaunti yoyote itapoteza fedha zozote katika mwaka huu wa kifedha wa 2020/2021.
Mnamo Jumanne wiki jana, maseneta wanaopinga mfumo ambao unaupa uzito idadi ya watu, ulikataliwa na maseneta wengi.
Hii ni licha ya Kiranja wa Wengi Irungu Kang’ata kupendekeza kuwa uanze kutumika baada ya miaka miwili, yaani katika mwaka wa kifedha wa 2022/2023.