• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
2022: Wanasiasa wachochea mauaji

2022: Wanasiasa wachochea mauaji

FRANCIS MUREITHI NA JOSEPH OPENDA

MAANDALIZI ya kuwania vyeo vya kisiasa kwenye uchaguzi mkuu wa 2022, yameibuka kuwa kiini kikuu cha mapigano ya kikabila ambayo yamesababisha kuuawa kwa watu watano, 80 kujeruhiwa na wengine 3,000 kuachwa bila makao katika Kaunti ya Nakuru kuanzia wiki iliyopita.

Kulingana na viongozi wa kijamii katika vijiji vinavyokumbwa na mapigano hayo katika maeneobunge ya Molo na Njoro, ghasia hizo zina uhusiano na zilizozuka majuzi katika eneo lilo karibu la Olposimoru, Kaunti ya Narok.

Mapigano hayo yanahusisha jamii ya Wakipsigis ambao ni wakulima waliohamia eneo hilo na kujistawisha kiuchumi kwa kununua ardhi, dhidi ya Wamasai.

Uchunguzi wa Taifa Leo mashinani ulibaini kuwa wengi wa jamii ya Wamasai wanahofia kuwa ongezeko la idadi ya watu wa jamii ya Wakipsigis kutoka kaunti jirani za Kericho na Bomet, ni tishio la kisiasa kwao hasa katika Narok ifikapo uchaguzi wa 2022.

Kufurushwa kwa jamii ya Ogiek kutoka Msitu wa Mau pia kumesababisha kuongezeka kwa joto la kisiasa kwani Ogiek wanalaumu jamii ya Wakipsigis kwa madai ya kuvamia msitu huo, ambao umekuwa tegemeo lao kiuchumi na kijamii tangu jadi.

KUKAMATWA

Hapo jana, Mshirikishi wa serikali kuu katika ukanda wa Rift Valley, George Natembeya alisema wanasiasa na maafisa wa utawala ni miongoni mwa washukiwa 16 ambao wamekamatwa kwa kuchochea na kushiriki kwenye mapigano hayo ya kikabila.

Maelfu ya watu pia wamelazimika kutoroka makwao karibu na Msitu wa Mau kufuatia ghasia hizo ambazo zimekumba vijiji 10 katika maeneobunge ya Molo na Njoro.

Kwenye kikao na wanahabari jana, Bw Natembeya alisema kati ya waliokamatwa ni naibu chifu wa Marioshoni. Washukiwa wanadaiwa kuwachochea wakazi kupigana baina yao.

Alisema washukiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo kufunguliwa mashtaka ya mauaji, uchomaji nyumba na uchochezi wa ghasia.

MAJERUHI

“Pia tunawachunguza watu zaidi, miongoni mwao maafisa wa utawala na wengine wanaolenga kuwania nyadhifa za kisiasa ambao wametajwa kuhusika katika mapigano hayo,” akasema Bw Natembeya.

Kati ya watu waliojeruhiwa, 40 wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali mbalimbali.

“Wale waliofariki wamo kati ya miaka 15 na 55 huku waliojeruhiwa wakiwa kati ya mwaka mmoja na miaka 35,” akasema Bw Natembeya.

Alieleza kuwa zaidi ya familia 3,000 zimeachwa bila makao baada ya nyumba 198 kuchomwa.

Familia zilizoachwa bila makao zinapiga kambi katika shule za msingi za Nessuit, Segekwa, Elburgon na Enatich.

Kulingana na Bw Natembeya, hali ya taharuki ilianza Jumanne usiku wiki iliyopita katika eneo la Marioshoni.

Bw Natembeya alisema kuwa serikali kwa ushirikiano na Shirika la Msalaba Mwekundu (KRCS) imeweka mipango ya kutoa chakula na mahitaji mengine ya kimsingi kwa familia zilizoathiriwa.

Alisema serikali itatoa mabati kwa familia zilizochomewa nyumba zao ili kuziwezesha kujenga nyumba mpya.

Bw Natembeya alisema serikali pia imeanza mazungumzo ya amani ili kupata suluhisho la kudumu kwa tatizo hilo.

Aliwaonya wanasiasa wakome kuchochea wakazi akiseman wanafanya uchunguzi wa kina kuhakikisha ghasia hizo zinakomeshwa.

You can share this post!

Wakazi wa Isiolo kupewa hatimiliki

Hawa ndio matapeli wa Kiswahili waliomkera Abdalla Mwasimba

adminleo