Wakuzaji miraa walia Somalia ikizuia ndege yenye tani 11 kutua
Na David Muchui
WAKULIMA wa miraa wamelalamika vikali baada ya ndege nyingine iliyobeba tani 11 za zao hilo kukatazwa kutua Somalia kwa dai kwamba ilipuuza kanuni za kuzuia virusi vya corona.
Hii ni ndege ya pili kurudishwa Kenya na serikali ya Somalia ikibeba miraa. Mwezi jana, ndege iliyokuwa imebeba tani 13 za miraa pia ilirudishwa Kenya.
Mwenyekiti wa chama cha wauzaji miraa cha Nyambene (Nyamita), Bw Kimathi Munjuri, alisema ndege hiyo ilitimiza kanuni zote na sheria za safari za ndege.
Alilaumu serikali ya Kenya akidai imepuuza kilio chao cha kuitaka izungumze na serikali ya Somalia kuhusu marufuku ya miraa nchini humo.
Somalia ilisimamisha biashara ya miraa mnamo Machi katika juhudi za kudhibiti msambao wa corona.
“ Ndege hiyo ilikuwa imebeba tani 11.3 za miraa aina ya Griid na Alele kupeleka Puntland. Ndege hiyo iliingia anga ya Djibouti mwendo wa saa nne mchana baada ya kupitia Ethiopia na ilikuwa ikijiandaa kutua Puntland ilipoagizwa kurudi Kenya. Hii ni ndege ya pili kurejeshwa Kenya katika muda wa mwezi mmoja,” akasema.