• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 7:50 AM
WANDERI: Ghasia za Nakuru zizimwe kabla ya hali kuzorota zaidi

WANDERI: Ghasia za Nakuru zizimwe kabla ya hali kuzorota zaidi

Na WANDERI KAMAU

MAPIGANO ambayo yamekuwa yakishuhudiwa katika maeneo ya Nessuit, Mariashoni na Ndoswa katika Kaunti ya Nakuru yanaachilia mwelekeo hatari wa kisiasa nchini.

Maeneo hayo yamo katika eneo la mashariki mwa Msitu wa Mau, ambao umekuwa ukikumbwa na utata mwingi tangu enzi za utawala wa marehemu Daniel Moi.

Mapigano haya yanahusisha jamii za Kipsigis na Ogiek, ingawa baadhi ya ripoti za kijasusi zinaeleza uwepo wa viongozi fulani wa kisiasa ndani ya mzozo huo.Kufikia sasa, inakisiwa watu watano wameuawa na zaidi ya 20 kujeruhiwa.

Bila shaka, mwelekeo huo ni hatari, ikizingatiwa eneo la Bonde la Ufa limekuwa ngome ya vita vya kikabila tangu miaka ya tisini.

Kile kinachozua wasiwasi zaidi ni kuwa hali hii inatokea wakati mielekeo ya kisiasa nchini pia inaendelea kuchukua mikondo mipya ya migawanyiko.

Kwa kurejelea historia kuhusu chimbuko na mielekeo ya ghasia za kikabila nchini tangu 1990, mwanzo wake huwa mzozo mdogo unaohusisha jamii moja ama mbili katika eneo husika kwa kiwango kidogo tu.

Hili mara nyingi hutokea mwaka mmoja ama miliwi kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika.Mzozo huo baadaye huenea na kuzihusisha jamii kadhaa katika eneo kubwa zaidi, huku wanasiasa wakianza kuingilia kati hali inapokuwa hatari zaidi.

Ni mwelekeo uliodhihirika kwenye ghasia za 1992 na 1997, huku upeo wa mapigano hayo ukiwa baada ya uchaguzi tata wa 2007. Kwa wakati huu wote, inashangaza hali hii haijawahi ‘kupata tiba,’ licha ya mikakati na juhudi mbalimbali ambazo zimewekwa kuikabili.

Kwenye ripoti yake 1997 kuhusu kiini cha ghasia za kikabila nchini, Jaji Mstaafu Akilano Akiwumi, alieleza kwa kina kiini cha mapigano na hata kuwataja baadhi ya wanasiasa ambao walikuwa wahusika wakuu.

Hata hivyo, wanasiasa wengi waliotajwa kuhusika walikuwa wakihudumu katika serikali ya Moi, hivyo ilikuwa vigumu kwa serikali waliyokuwa wakitumikia kuwachukulia hatua.

Zaidi ya hayo, wengi walionekana kuwa nguzo kuu kwa Moi kuendelea kupata uungwaji mkono katika eneo hilo.Kama ilivyo kawaida nchini, ripoti hiyo haijawahi kutekelezwa wala wahusika wakuu kuchukuliwa hatua za kisheria.

Baada ya ghasia za 2007, miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni kubuniwa kwa Tume ya Haki, Ukweli na Maridhiano (TJRC), iliyoongozwa na Balozi Bethwel Kiplagat.

Kama Jaji Akiwumi, lengo kuu la tume lilikuwa kuchunguza madhila ya kijadi tangu 1963, kuwataja wahusika wakuu na kutoa mapendekezo kuhusu ushughulikiaji wake.

Tume ilizunguka katika sehemu mbalimbali nchini na kupokea maoni kutoka kwa Wakenya kuhusu kila aina ya dhuluma ambazo wamepitia tangu utawala wa Mzee Jomo Kenyatta.

Licha ya serikali kukabidhiwa ripoti, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kuwaadhibu waliotajwa kuhusika.Kama miaka ya awali, tuko katika hali ya hatari.

Kuna uwezekano maafa kushuhudiwa tena 2022 ikiwa hatutasoma nyakati kutokana na matukio ya awali kama ilivyo sasa Nakuru na kuchukua hatua za kuzuia hali kuzorota [email protected]

You can share this post!

Malala amchemkia Oparanya kwa kupuuza vijana

WASONGA: Mzozo wa ugavi pesa ni kuhusu siasa wala si...

adminleo