• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
WASONGA: Mzozo wa ugavi pesa ni kuhusu siasa wala si maslahi ya raia

WASONGA: Mzozo wa ugavi pesa ni kuhusu siasa wala si maslahi ya raia

Na CHARLES WASONGA

LEO maseneta wanarejelea mjadala tata kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha miongoni mwa kaunti 47. Hii ni baada yao kukosa kuelewana Jumanne iliyopita.

Kiranja wa Wengi Irungu Kang’ata, kama kawaida yake, kwa mara nyingine ameelezea kujitolea kwa mrengo wa serikali kuhakikisha kuwa mfumo uliopendekezwa na Kamati ya Seneti kuhusu Fedha unapitishwa.Mfumo huo ni zao la marekebisho yaliyofanyiwa kwa mfumo uliopendekezwa na Tume ya Ugavi wa Mapato (SRC) ambao unapatia uzito kigezo cha idadi ya watu.

VUTA nikuvute hii inayochochewa na dhana kwamba mfumo unaopendekezwa unaziongozea kaunti tajiri fedha kwa kuzipokonya kaunti maskini haina maana yoyote wala manufaa kwa raia wa kawaida.

Suala muhimu ambalo maseneta wanapasa kulishughulikia kwa kina ni iwapo fedha ambazo tayari kaunti hizo zimepokea zilitumika kwa manufaa ya wakazi wa kaunti husika au la.

Maseneta ambao wanachangamkia mfumo uliopendekezwa, kwa misingi kwamba utapelekea kaunti zao kupokea fedha zaidi, wanafaa kwanza kuthibitisha namna ambavyo wamelinda pesa ambazo kaunti hizo zimepokea tangu 2013.

Vivyo hivyo, wale ambao wanalalama kuwa kaunti zao zitapokonywa fedha waelezee hatua ambazo wamechukua kuzuia ubadhirifu na wizi wa fedha chache ambazo kaunti hizo zimekuwa zikipokea kabla ya kudai kuzitetea zisipokonywe fedha.

Kulingana na kipengele cha 96 cha Katiba, ni wajibu wa Seneti kulinda masilahi ya kaunti, zikiwemo fedha ambazo hugawiwa kaunti hizo kutoka hazina ya kitaifa.

Kwa hivyo, ni wajibu wa maseneta kuhakikisha kuwa fedha zinazotengewa kaunti zote 47 zinatumiwa kwa shughuli zilizokusudiwa na zenye manufaa kwa raia.

Lakini ripoti za kila mwaka za Mkaguzi wa Mkuu wa Matumizi ya Fedha za Umma na Msimamizi wa Bajeti (CoB) ambazo hufichua visa vya wizi na ubadhirifu wa mabilioni ya fedha za umma ni ithibati tosha kwamba maseneta hawajakuwa wakitekeleza wajibu wao ipasavyo.

Kwa hivyo, mvutano wa sasa kuhusu kaunti zitakazopoteza fedha au zile zitakazofaidi hauna maana yoyote kwa “Wanjiku”, ambaye ndiye mwathirika katika sakata za wizi wa fedha za umma.

Maseneta wanahadaa kwamba wanatetea masilahi ya wananchi katika kaunti zao, ilhali ukweli ni kwamba wanatetea masilahi yao ya kisiasa.Kwa mfano, maseneta kama vile Mutula Kilonzo Junior (Makueni) na Ladema Ole Kina (Narok) wanapinga mfumo huo ulipendekezwa kwa sababu utaathiri ndoto zao za kurithi viti vya ugavana katika kaunti zao hapo 2022.

Hali ni sawa kwa wenzao Samson Cherargei (Nandi) na Kimani wa Matangi (Kiambu) wanaounga mkono mfumo huo unaongezea kaunti zao fedha ili wapate kigezo cha kutumia wakisaka kura za ugavana katika kaunti zao.

You can share this post!

WANDERI: Ghasia za Nakuru zizimwe kabla ya hali kuzorota...

‘Corona ilinisukuma kugeuza shule yangu vyumba vya...

adminleo