• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Wito mapigano ya kikabila yakomeshwe

Wito mapigano ya kikabila yakomeshwe

Na SAMMY WAWERU

Boma likiwa na ukwasi wa kutosha lakini likose amani mazingira yake huwa mithili ya pango la simba, ambalo kwa binadamu halikaliki.

Taifa likiwa na raslimali chungu nzima, amani ikose, halitakalika na utajiri huo hautawafaa raia na hakuna maendeleo yatakayofanyika.

Wiki iliyopita, machafuko na ghasia zilishuhudiwa eneo la Njoro, Kaunti ya Nakuru, kufuatia mzozano wa kijamii uliosababisha maafa ya watu kadhaa.

Mzozano huo wa kikabila ulianza mnamo Julai 28, 2020, usiku, eneo la Olposimoru.

Vita hivyo vimesambaa hadi maeneo ya Nassuit, Ndosua na Marioshoni, yote yakiwa Njoro, ambapo mbali na maafa, watu kadhaa wamejeruhiwa vibaya na nyumba kuteketezwa moto.

Kufuatia mizozano hiyo, Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui alitangaza kuweka kafyu kati ya saa kumi na mbili za jioni na saa moja asubuhi muda wa siku tano mfululizo kuanzia Julai 31, itakayotekelezwa eneo la Njoro, Mau Narok na Elburgon, ili kusaidia kuzima vita hivyo.

Amri hiyo imejiri wakati ambapo kafyu ya kitaifa, kati ya saa tatu usiku na saa kumi alfajiri, iliyowekwa kusaidia kuzuia msambao wa virusi vya corona (Covid-19) inaendelea kutekelezwa.

“Wakazi wote wanashauriwa kutii sheria za nchi. Atakayezikiuka mkono wa sheria utachukua mkondo wake,” Gavana Kinyanjui akaonya, baada ya kutembelea manusura wa vita hivyo katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Nakuru.

Watu kadhaa wanaoshukiwa kuwa wachochezi wa vita hivyo vinavyosemekana kuchangiwa na siasa wametiwa nguvuni, Mshirikishi wa Bonde la Ufa George Natembeya akisema kuwa wahusika watachukuliwa hatua kisheria.

Mzozano huo wa kikabila Njoro, na mingine inayoshuhudia katika maeneo kama vile Narok, Baringo, Pokot, Turkana, na Laikipia, na mengineyo, ni ishara ya wenyeji kukosa kuthamini amani.

Licha ya kuwa inahusishwa na mivutano ya mifugo na umiliki wa ardhi, vita hivyo vinaashiria wakazi wanahitaji hamasisho la kina na la kutosha kuhusu amani.

Kina cha amani

Amani, maanaye ni hali ya raha na salama bila ugomvi. Pia, ni hali ya kutokuwa na vita kati ya familia, makundi, jamii, au nchi, kwa sababu vita huleta uharibifu mkubwa wa mali na hata uhai.

Fujo za mara kwa mara katika maeneo hayo zimelemaza maendeleo na mambo mengine makuu kwa wenyeji, kwa ajili ya ukosefu wa neno au nomino AMANI.

Mto au maji yanayotiririka, ukifuata mkondo wake, yana kiini. Hii ina maana kuwa fujo za maeneo hayo zina chanzo. Huenda ikawa ni chocheo la wanasiasa, mvutano wa umiliki wa ardhi au mashamba, wizi wa mifugo, kati ya vijisababu vingine na ambavyo vimewanyima amani.

Ni muhimu ifahamike ni haki kisheria kila Mkenya kuishi kwa amani na katika mazingira salama. Isitoshe, ndio maana kuna asasi ya usalama.

Kulingana na Ronald Korir, mchanganuzi wa masuala ya kiusalama, serikali inapaswa kuwekeza kwa kiwango kikuu hamasisho la umuhimu wa kudumisha amani eneo la Njoro na mengine yanayoshuhudia fujo na vita vya kijamii vya mara kwa mara.

Mdau huyo anasema huenda ikawa kazi bure kutuma vikosi vya usalama kukabiliana na mtandao wa magenge ya wahuni wanaozua rabsha, akisema maafisa wa usalama hawataishi humo nyakati zote.

Korir anasema busara ni kufanya oparesheni kujua kiini cha migongano hiyo, hatua inayopaswa kushirikisha au kuhusisha wakazi, wazee wa kijiji na viongozi wa kisiasa na wa kidini maeneo hayo.

Hali kadhalika, mchanganuzi huyo anasema serikali ilenge kundi la vijana na ambao mara kwa mara huchochewa kufanya uvamizi.

“Kiwango chao cha kutafakari mambo ni cha chini mno. Ili kumaliza ghasia hizo, serikali ifanye hamasa kuhubiri amani na iwahami kwa maarifa kuelewa umuhimu wa amani. Hiyo ni mojawapo ya njia kutafuta suluhu ya kudumu maeneo hayo,” Korir anashauri, pia akihimiza haja ya kutilia mkazo elimu miongoni mwa vijana.

Ni maeneo yaliyojaaliwa raslimali chungu nzima, hasa udongo wenye rutuba kufanya kilimo, ila ghasia zinazotukia zinawakosesha amani. “Wakifahamu amani ndiyo nguzo ya ufanisi na maendeleo, hakuna atakayekubali kutumika kuzua vita,” Korir anaeleza.

Ndio, serikali inaonekana kujaribu kuzima mizozano hiyo, ila inapaswa kujua amani itapatikana wenyeji wakiitikia kuishi kama ndugu na dada, na kuzika katika kaburi la sahau ukabila. Wanawake, kina mama na watoto ndio huumia kwa kiwango kikuu fujo zinapozuka.

You can share this post!

Kenya Power matatani baada ya mama na mwanawe kuuawa na...

Majitaka yatia wakazi wasiwasi

adminleo