Toka ODM tuunde chama chetu, Jumwa amsihi Kingi
CHARLES LWANGA na FARHIYA HUSSEIN
MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa amemtaka Gavana wa Kilifi Amason Kingi aunge wito wa wabunge wa Pwani kuuganisha wakazi kwa ajili ya kuunda chama cha siasa kitakachotumika katika uchaguzi wa 2022.
Mbunge huyo ambaye ameasi chama cha ODM anamtaka Bw Kingi aunge wito huo bila hofu, ili Pwani ijikwamue kutoka kwa udhibiti wa kinara wa ODM Raila Odinga.
“Gavana Kingi toa shaka, toa hofu na uungane nasi. Safari ya kuunganisha Wapwani imeng’oa nanga. Sisi viongozi wa Pwani na wakazi tumejipanga na hakuna kurudi nyuma,” alisema wikendi katika mkutano mjini Malindi.
Mwanzoni mwa mwaka wa 2018, Bw Kingi ambaye ndiye mwenyekiti wa chama cha ODM katika kaunti ya Kilifi, aliwakashifu wabunge wa ODM katika mrengo wa ‘Tangatanga’ akisema wao ni wasaliti kwa kuitisha umoja wa Wapwani, huku wakimpigia debe Naibu Rais William Ruto kuwa rais mwaka wa 2022 badala ya kiongozi wa Pwani.
Wabunge wengine ambao wameungana na Bi Jumwa kuuganisha Wapwani kwa nia ya kuunda chama ni Mohammed Ali (Nyali), Michael Kingi (Magarini), Owen Baya (Kilifi Kaskazini), Sharif Ali (Lamu Mashariki), Andrew Mwadime (Mwatate), Khatib Mwashetani (Lunga Lunga), Jones Mlolwa (Voi), Paul Kahindi (Kaloleni) na Benjamin Taya (Kinango).
Lakini wiki jana, Katibu Mkuu wa Chama cha ODM, Bw Edwin Sifuna alipuuzilia mbali madai ya wabunge hao akisema kuwa wengi wao si wa ODM na wachache waliosalia walifukuzwa chamani au wamekuwa katika mrengo wa ‘Tangatanga.’
Bi Jumwa alisema kuwa viongozi wa Pwani ambao wameanza shughuli ya kuuganisha wakazi na kuunda chama hawana nia ya kumsimamisha mwaniaji wa urais kutoka maeneo mengine ya nchi.
“Nia yetu ni kuwa na gari letu la siasa litakalotupa nguvu bungeni katika miswada kama ile ya ugavi wa rasilimali na uongozi,” alisema.
Hata hivyo, mbunge wa Mvita, Abdulswamad Nassir amewashutumu vikali wenzake wa Pwani wanaotishia kuhama ODM. Akizungumza na Taifa Leo, alimtetea Bw Odinga na kusema wanasiasa hao si waaminifu kwa chama.
‘Watu hawa hawajawahi kuwa waaminifu kwa chama. Baadhi yao hata hawapo kwenye chama cha ODM. Kwa hivyo sielewi ni kwa nini wanaendelea kutaja ODM,’ akasema.
Kulingana na mbunge huyo, viongozi hao wanaopanga kuunda chama kipya, walikuwepo wakati wa mkutano wa ripoti ya BBI na wote wakapata nafasi ya kutoa maoni yao.
Kulingana na baadhi ya viongozi, uamuzi wa Bw Odinga kuunga mkono mswada tata wa ugawaji wa mapato uliwakasirisha viongozi wa Pwani.
Hii ndiyo sababu mojawapo iliyoshinikiza baadhi ya viongozi akiwemo mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya ambaye amekuwa kwenye mstari mbele kuunga mkono uzinduzi wa chama kipya cha siasa kuunganisha Wapwani.