Habari Mseto

Ujenzi wa daraja la watu pekee waanza Likoni

August 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

MOHAMED AHMED na CECE SIAGO

MSONGAMANO katika kivuko cha Likoni unatazamiwa kupungua hivi karibuni kufuatia kuanza kwa ujenzi wa daraja la watu pekee ambalo linajengwa kwa gharama ya Sh1.5 bilioni.

Ujenzi wa daraja hilo la kuelea umeanza eneo la Liwatoni upande wa Mombasa kisiwani na utamalizikia upande wa Likoni eneo la Peleleza.

Kazi imeanza kwa wiki moja sasa baada ya tume ya ardhi ya NLC kuchukua ardhi kutoka kwa wamiliki wa eneo hilo la Liwatoni baada ya mashauriano.

Mradi wa daraja hilo unatazamiwa kupambana na msongamano wa mara kwa mara katika kivuko cha Likoni ambacho kinatumiwa na watu zaidi ya 320, 000 kwa siku.Misongamano ya watu na magari imekuwa ikishuhudiwa kwa sababu ya kuharibika kwa feri kivukoni hapo.

Hivi majuzi, watu zaidi ya 20 walijeruhiwa baada ya mkanyagano uliosababishwa na kuondolewa kwa feri mpya ya Mv Safari.

Feri hiyo ya Mv Safari iliondolewa baada ya kugongwa na ile ya Mv Kwale. Kufikia sasa feri hiyo ya Mv Safari haijarudishwa kazini.

Kuhusiana na ujenzi wa daraja, msimamizi wa sehemu ya ujenzi huo Bw Evans Momanyi ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Sakawa Agencies Limited alisema kuwa sehemu ambayo itashikilia vyuma vya daraja hilo utamalizika mwisho wa mwezi huu.

“Tumeweka wafanyakazi wetu na vifaa hitajika ili kuhakikisha kuwa kazi hii inamalizika wakati mwafaka. Daraja hili litaunganishwa na barabara ya eneo hili la Liwatoni ambapo abiria atatembea kidogo kabla afike kwenye daraja lenyewe,” akasema.

Daraja hilo litakuwa na upana wa mita sita na urefu wa mita 529 na kutoka upande wa Mombasa kisiwani na kuvuka bahari hadi upande wa Likoni.

Katikati ya daraja hilo kutakuwa na sehemu ambayo inafunguka ili kuruhusu meli na vyombo vyingine vya baharini kupita.Meli zinazoingia bandarini Mombasa hutumia sehemu hiyo ya kivuko cha Likoni ambapo daraja hilo litawekwa.

Akizungumza alipotembelea eneo hilo la ujenzi, Mshirikishi wa Pwani, Bw John Elungata, alisema daraja hilo litasaidia kukabili msongamano kivukoni.Haya yanajiri huku wakazi wa Mtongwe wakitishia kuandamana kwa kuchelewa kurejeshewa huduma za feri.

Zaidi ya watu 10,000 watalazimika kutumia feri ya upande wa Likoni, ambako tayari zaidi ya watu 300,000 husongamana kila siku.

Huduma za feri katika kivuko cha Mtongwe zilisimamishwa Septemba mwaka jana, kwa muda wa miezi sita ili kukamilisha ujenzi wa mradi wa Sh20 milioni.

Hata hivyo, huduma hizo hazikurejea mwezi Machi kama ilivyotarajiwa, na sasa wakazi wanatishia kuandamana ili kushinikiza shirika la Kenya Ferry kurejesha safari.