Habari MsetoSiasa

Ruto aunga mkono 'Team Kenya'

August 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto Ijumaa, Agosti 7, aliunga mkono mifumo iliyopendekezwa na maseneta Johnson Sakaja (Nairobi) na Mithika Linturi (Meru) ya ugavi wa fedha baina ya kaunti.

Kwenye taarifa kupitia akaunti yake ya Twitter, Dkt Ruto alielezea matumaini kuwa muafaka unaelekea kupatikana kupitia mapendekezo ya maseneta hao wawili.

“Makubaliano yanayoelekea kufikiwa na Sakaja na Linturi kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha ambapo kaunti zenye watu wengi zitapokea nyongeza kidogo na zingine zikipunguziwa kiwango cha fedha ambazo zingepoteza, ni hatua bora ya kuonyesha dalili za kupatikana kwa makubaliano”.

“Seneti iliyoungana kwa moyo wa uzalendo itapata suluhu la kudumu kuhusu suala hili tata,” Naibu Rais Dkt Ruto akaeleza.

Kundi la maseneta waliopinga mfumo uliopendekezwa na Kamati ya Seneti kuhusu Fedha na linalojiita, “Team Kenya” lilisema linaunga mkono mapendekezo ya Sakaja na Linturi.

Pendekezo la Linturi linadumisha vigezo vilivyoko katika mapendezo ya awali ya Sakaja, japo linapunguza idadi ya fedha ambazo zitapasa kugawanywa kwa misingi ya mfumo wa mwaka jana.

Kiasi hicho cha fedha ni kati ya Sh250 bilion na Sh270 bilioni kati ya Sh316.5 zilizotengewa serikali 47 za kaunti katika bajeti yam waka huu wa kifedha wa 2020/2021. Kiasi kamili cha fedha kitafikiwa baada ya mazungumzo kukamilishwa Jumatatu, Agosti 10.

Bw Linturi anapandekeza kuwa fedha zitakazosalia zigawanywe kwa misingi takwimu za matokeo ya sensa ya mwaka wa 2019, ambazo ndizo zilizingatiwa katika mfumo uliopendekezwa na Kamati ya Seneti kuhusu Fedha.

“Fedha zozote zaidi ya kiasi ambacho kitakubaliwa kuwa zigawanywe chini ya mfumo wa mwaka jana, zitagawanywa kwa kuzingatia mfumo uliopendekezwa na Kamati ya Fedha inayoongozwa na Seneta wa Kirinyaga Charles Kabiru,” akasema Bw Linturi ambaye ni Seneta wa Meru na mmoja wa wanachama wa kundi la Tangatanga linalovumisha azma ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022.

Mnamo Jumanne Agosti 4, mjadala kuhusu suala hilo ulikatizwa katika Seneti baada ya maseneta wengi kuunga mkono hoja ya Murkomen kwamba wapewe muda zaidi wa kusaka muafaka.

“Naamini kuwa tunaweza kukubaliana kuhusu mfumo ambapo hakuna kaunti itapoteza. Mfumo utakaowezesha kaunti zote kushinda na hivyo kudumisha umoja wa nchini. Hatutaki nchi ya igawanyika kwa misingi ya waliopoteza na waliofaidi,” akasema Bw Murkomen.