Michezo

HAWANA BAHATI: Barcelona na Bayern Munich kukabiliana katika robo fainali

August 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

BARCELONA, UHISPANIA

OLE wao! Mmoja kati ya majabali wa soka duniani; Barcelona na Bayern Munich, hatashiriki nusu fainali ya kabumbu ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Kisa na maana? Miamba hao wanakutana katika robo fainali baada ya kung’aa katika hatua ya 16-bora Jumamosi usiku.

Barcelona walijikatia tiketi ya kuvaana na Bayern kwa mara ya 13 mfululizo baada ya kuwapepeta Napoli 3-1 uwanjani Camp Nou kwa jumla ya mabao 4-2.

Bayern nayo ilipiga hatua hiyo baada ya kuibwaga Chelsea kwa kuilima 4-1 (jumla ya 7-1) jijini Munich, Ujerumani.

Katika mechi nyinginezo za robo-fainali, Atalanta ya Italia itapimana ubabe na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa huku RB Leipzig ya Ujerumani ikionana na Atletico Madrid ya Uhispania.

Manchester City waliowadengua Real Madrid kwenye hatua ya 16-bora, watakabiliana na Olympique Lyon iliyowabwaga miamba wa soka ya Italia, Juventus.

Mabao ya Barcelona dhidi ya Napoli yalifumwa wavuni na Clement Lenglet, Lionel Messi na Luis Suarez katika kipindi cha kwanza kilichotawaliwa na matukio mengi ya utata hadi ikalazimu VAR itumike.

Barcelona walijitosa ugani kwa minajili ya mechi hiyo wakijivunia bao la ugenini katika sare ya 1-1 waliyolazimishiwa na Napoli katika mkondo wa kwanza nchini Italia mnamo Februari 2020.

Lenglet aliwafungulia Barcelona ukurasa wa mabao katika dakika ya 10 kabla ya Messi kufunga la pili dakika 13 baadaye.

Bao la tatu la Barcelona lililojazwa kimiani na Suarez lilitokana na penalti iliyochangiwa na Kalidou Koulibaly kumchezea Messi visivyo dakika ya 44.

Ivan Rakitic alimkabili Dries Mertens visivyo mwishoni mwa kipindi cha kwanza na kusababisha penalti ambayo Napoli walifungiwa na Lorenzo Insigne.

“Huu ndio mtihani uliokuwa muhimu zaidi kwetu. Baada ya kuupita, ni matumaini yangu kwamba tutajizatiti vilivyo kwa kibarua kilichopo mbele na hatimaye kunyanyua ufalme wa UEFA kwa mara ya kwanza tangu 2015. Hili ni jambo linalowezekana iwapo vijana wataendeleza ari waliyoidhihirisha dhidi ya Napoli katika mechi zote zilizosalia,” akasema kocha Quique Setien wa Barcelona.

Kabla ya mechi dhidi ya Napoli, Setien alikuwa amekiri kwamba kubanduliwa kwa Barcelona kwenye hatua ya 16-bora ya UEFA kungemning’iniza pembamba zaidi ugani Camp Nou.

Kiini cha Barcelona kumwajiri mkufunzi huyo wa zamani wa Real Betis kujaza pengo la Ernesto Valverde ni kutambisha miamba hao katika soka ya Uhispania na bara Ulaya. Hata hivyo, chini ya ukufunzi wake, Barcelona walishindwa kuhifadhi ubingwa wa La Liga msimu huu na wakabanduliwa kwenye robo-fainali za Copa del Rey.

Japo Barcelona hawajawahi kushindwa kufuzu kwa robo-fainali za UEFA tangu 2007, kibarua kizito zaidi kwao ni jinsi ya kuzima makali ya Bayern.

Mechi zote zilizosalia ni za mkondo mmoja pekee na zitachezwa nchini Ureno kati ya Agosti 15-19. Fainali itatandaziwa jijini Lisbon, Ureno, Agosti 23.

Ratiba ya Robo fainali: Atalanta na PSG (Agosti 12), RB Leipzig na Atletico (Agosti 13), Barcelona na Bayern (Agosti 14), Man-City na Lyon (Agosti 15).