Huu ni mzaha tu!
Na TAIFA RIPOTA
MAAFISA wakuu serikalini wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, wameendelea kuvunja kanuni walizoweka wenyewe za kukabili kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona.
Ingawa wanafahamu misongamano ni moja ya njia zinazochangia pakubwa kusambaa kwa virusi hivyo hatari, viongozi hao wamekuwa wakikupuuza tahadhari ya Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Kwao binafsi wanakaa mbali na watu na kuvaa barakoa, lakini hawatalii maanani hatari wanayoweka wananchi wanaohutubia.
RAIS KENYATTA
Mnamo Jumatatu, Rais Kenyatta alihutubia umati uliosongamana alipokuwa akizindua ujenzi wa hospitali katika mitaa ya mabanda ya Uthiru, Kibra na Mukuru jijini Nairobi.
Hii ni licha ya kuwa Rais mwenyewe ndiye aliyetangaza marufuku ya mikusanyiko ya watu wengi, kulingana na ushauri wa wataalamu kuwa virusi vya corona vinasambaa kwa urahisi mahala kuna misongamano ya watu.
“Kwa ushauri wa Baraza la Kitaifa la Usalama na Kamati ya Dharura kuhusu janga la corona, naagiza kuongezwa kwa muda wa marufuku ya mikusanyiko aina yoyote ile kwa siku 30 zaidi,” akasema Rais Kenyatta alipohutubia taifa mnamo Julai 6.
Lakini hilo halikumzuia kiongozi wa nchi kuvunja sheria na kuhatarisha maisha ya mamia ya watu waliokusanyika kumsikiza, hali ambayo inachangia ongezeko la maambukizi nchini kila siku.
Alipohutubia taifa mnamo Julai 27, Rais alisisitiza kuwa hatua alizotangaza zinapasa kuheshimiwa na kila Mkenya bila kujali hadhi yake katika jamii.
“Maafisa wa utawala na polisi watatekeleza kikamilifu kanuni za Wizara ya Afya kuhusu mikutano ya umma. Inspekta Jenerali wa Polisi atahakikisha kuwa maafisa wake hawatasaza yeyote, awe mheshimiwa ama mtu binafsi, ambaye atavunja kanuni za afya, bila kujali cheo chake,” akasema Rais mnamo Julai 27.
KAGWE
Bw Kagwe naye amegeuka kuwa mhubiri anayewahimiza watu kunywa maji lakini yeye mwenyewe anabugia mvinyo.
Hii ni baada ya waziri huyo kuhutubia halaiki ya watu katika eneo la Ainamoi, Kaunti ya Kericho alipokuwa akikagua maandalizi ya kupambana na Covid-19.
Ilikuwa kinaya kwa Bw Kagwe kwenye hotuba yake kuwaambia wakazi hao kutii kanuni za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona huku akijionea mwenyewe hawakuwa wakiheshimu hitaji la kuepuka misongamano.
“Nawahimiza muendelee kutii kanuni za Covid-19 ili kuzuia maambukizi zaidi,” akasema Bw Kagwe hali akijionea kuwa hadhira yake haikuwa ikizingatia kanuni hizo.
Waziri Kagwe kwenye hotuba zake kwa taifa amekuwa mstari wa mbele kuhimiza Wakenya kuepuka maeneo yenye watu wengi, akisema hali hiyo inachangia zaidi maambukizi.
Pia wizara yake imekuwa ikiendesha kampeni kwenye vyombo vya habari kuhimiza watu kuepuka misongamano, na ni jopo lake lililoshauri Rais kuhusu kuongeza muda wa marufuku ya mikusanyiko.
Katika kuzuia misongamano, Serikali ilitoa masharti makali ya shughuli za kidini, mazishi, uchukuzi wa umma na kuagiza kufungwa kwa mabaa kote nchini.
Lakini mnamo Jumatatu waziri alikiuka kanuni kwa kukubali kuhutubia watu waliokuwa wakivunja kanuni za wizara yake.
NATEMBEYA
Mshirikishi wa shughuli za serikali katika eneo la Rift Valley, George Natembeya naye amekuwa akikiuka kanuni za mikusanyiko mara kwa mara.
Wiki iliyopita, Bw Natembeya aliongoza mkutano uliohudhuriwa na mamia ya watu katika eneo la Nessuit, Kaunti ya Nakuru katika juhudi za kutafuta mwafaka wa amani kati ya jamii mbili ambazo zimekuwa zikizozana.
Kwenye mkutano huo watu walisongamana na hakukuwa na umbali uliowekwa, huku baadhi wakikosa kuvaa barakoa kama ambavyo serikali imekuwa ikihimiza.
Hii ni licha ya kuwa kamishna huyo ni miongoni mwa wakuu ambao wanapasa kuwa katika mstari wa mbele kuhakikisha kanuni za Wizara ya Afya kuhusu Covid-19 zinaheshimiwa na wote.
Mnamo Juni 26, Bw Natembeya na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Edward Mbugua waliongoza mkutano mwingine ulioshuhudia msongamano mkubwa katika eneo la Ol-Lessos katika Kaunti ya Nandi. Wengi wa waliokuwemo hawakuwa wamevaa barakoa.
Awali Juni 22, 2020, Bw Natembeya na Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui walihutubia mkutano mkubwa katika eneo la Likia, ambapo wengi wa waliohudhuria hawakuwa wamevaa barakoa.
Uvunjaji huu wa kanuni ambazo wanaozikiuka ndio wameweka, zimewakera Wakenya wengi wanaoona kuwa wakuu wa serikali hawako makini kukabiliana na janga la Covid-19.